SERIKALI YATOA MILIONI 500 KUJENGA KITUO CHA AFYA KASANSA
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) ameahidi kutoa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa Kituo cha Afya Kata ya Kasansa ili kusaidia wanachi wanaotembea umbali mrefu kutafuta huduma za afya.
Mheshimiwa Ummy alitoa ahadi hiyo jana Julai 16 2021 alipotembelea kata hiyo iliyopo umbali wa takribani kilomita 68 kutoka makao makuu ya wilaya; na zaidi ya kilomita 160 kutoka makao makuu ya Mkoa wa Katavi.
Mheshimiwa Ummy alisema kuwa yeye na wataalamu kutoka wizarani wameguswa sana kuona wananchi wa Kasansa na hasa wakinamama wanapata shida sana kwa kutembea takribani kilomita 25 kutafuta huduma ya Afya na kuahidi kuwaunga mkono.
“Ndugu zangu Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuboresha huduma za Afya Msingi na hasa huduma ya Mama na Mtoto. Hivyo kwa niaba ya Rais ninaahidi kuleta shilingi milioni 500 kwa ajili ya kujenga kituo cha Afya hapa, “ alisema Ummy.
Aidha pamja na fedha hizo za ujenzi wa kituo cha Afya, alisema kuwa mara baada ya kukamilika Serikali italeta shilingi milioni 300 kwa ajili ya vifaa tiba.
Awali Mhe. Geofrey Pinda mbunge wa jimbo la Kavuu (naibu waziri wa Katiba na sheria) ambaye kata hiyo ipo jimboni kwake, alimueleza waziri kuwa zahanati yao imezidiwa na wanauhitaji Mkubwa wa kituo cha Afya.
“Kwakweli mheshimiwa waziri wakinamama wanapata tabu sana zahanati imezidiwa na ili kupata huduma ya rufaa inawalazimu kutembea takribani kilomita 27 kutafuta huduma katika kituo cha Afya cha Mamba,” alisema Pinda.
Naye Diwani wa Kata (Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Mpimbwe,} Mhe. Sailas Ilumba alimshuku waziri Ummy na kusema ujio wake ni faraja na matumaini kwao kwa kua kero za wananchi zitapata ufumbuzi.
Post a Comment