Rwanda na Congo yapewa onyo la Mwisho na Marekani
Marekani imezionya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kutaka zijizuie na zirudi nyuma ili kuepusha kutumbukia katika vita wakati huu ambao hali ya wasiwasi ikiongezeka kati ya Nchi hizo jirani.
Onyo la Marekani limetolewa na Naibu Balozi wake katika Umoja wa Mataifa Robert Wood katika kikao cha dharura cha Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Congo kilichoitishwa na Ufaransa Jijini New York wakati huu ambao hali ya machafuko ikizidi kuwa mbaya eneo la mashariki mwa Congo linalopakana na Rwanda.
Wood alisema Rwanda na Congo, pamoja na Wadau wengine wa ukanda huo wanatakiwa mara moja waanzishe tena mazungumzo ya kidiplomasia na kusisitiza kuwa juhudi hizi za kidiplomasia ndio njia pekee kuelekea kupata suluhisho la pamoja na amani ya kudumu na sio kupitia harakati za kijeshi.
Wood amenukuliwa akisema “Rwanda lazima ifikishe mwisho kutoa msaada kwa Waasi wa M23, lazima pia iviondoe Vikosi vyake kutoka ardhi ya Congo na iondoshe mifumo yake yote ya makombora ya kutokea ardhini kwenda angani, ripoti za kuaminika zinaashiria Waasi wa M23 wamehusika kuvishambulia kwa makusudi na makombora vifaa vya Tume ya Amani ya Umoja wa Mataifa vilivyopo angani”.
Kwa mujibu wa DW, onyo la Marekani linafuatia hatua ya Wizara ya mambo ya nje ya Rwanda kukataa miito ya Marekani siku ya Jumatatu ya kuondoa Vikosi vyake na mifumo ya makombora ya angani kutoka mashariki mwa Congo.
Balozi wa Congo katika Umoja wa Mataifa, Zenon Ngay Mukongo, amelihimiza Baraza la usalama liitake Rwanda iviondoshe vikosi vyake vyote kutoka Congo bila masharti yoyote na isitishe msaada wote kwa Kundi la M23 ambapo amelituhumu Jeshi la Rwanda kuikalia sehemu ya jimbo la Kivu Kaskazini kwa njia isiyo halali na kuwasaidia Waasi hao kwa lengo la kuiyumbisha Congo na kupora utajiri wao wa madini.
Post a Comment