Lowassa amefariki dunia


 Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa (70) amefariki dunia leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, Dar es Salaam.


Taarifa ya kifo chake imetangazwa na Makamu wa Rais, Dkt. Philip Mpango. 


Rais wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza siku tano (5) za maombolezo ambapo bendera zitapepea nusu mlingoti kuanzia leo Februari 10, 2024 kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa kilichotokea leo. 


“Ninaungana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan katika maombolezo kufuatia kifo cha Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Edward Ngoyai Lowassa.”


“Kwa hakika nchi yetu imepata pigo kubwa kutokana na msiba huu mzito, kwakuwa Mhe. Edward Lowassa alikuwa Kiongozi aliyehudumu kwa juhudi na maarifa makubwa katika nafasi zote alizowahi kuzishika ikiwemo ya Uwaziri Mkuu.”


“Natoa pole kwa Familia, Wanamonduli na Watanzania wote kwa msiba huu na Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema, Amen!”—Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa.



Mazishi ya Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Edward Lowassa yanatarajiwa kufanyika Februari 17, 2024 kijijini kwao Ngarash wilayani Monduli Mkoa wa Arusha.


Taarifa kuhusu maziko yake,

iliyotolewa leo Februari 11, 2024 na msemaji binafsi wa Lowassa, Aboubakar Liongo nyumbani kwa mwanasiasa huyo, Masaki jijini Dar es Salaam imebainisha kuwa ratiba rasmi ya mazishi itaanza Februari 13, 2024 itakayohusisha taratibu zote za kiserikali.


Taarifa hiyo imeeleza kuwa waombolezaji wataondoka Dar es salaam kuelekea Arusha siku ya Alhamisi ambapo msiba utahamia Arusha.


Lowassa alifariki Dunia Februari 10, 2024 majira saa 8 mchana katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu.


Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango jana, Lowassa alifikishwa katika taasisi hiyo baada ya kuugua shinikizo la damu, matatizo ya mapafu na

kujikunja kwa utumbo.


"Taarifa zaidi kuhusu mazishi itatolewa baadaye, lakini kwa sasa maziko yatafanyika Ngarash Monduli mkoani Arusha siku ya Jumamosi, Februari 17, 2024 saa 8 nmchana," amesema Liongo.

No comments