MKATABA WA HUDUMA KWA MTEJA NI MUHIMU WA WANANCHI

Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali watu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bw. Victor Kategere amesema mkataba wa huduma kwa mteja utasaidia kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi na wadau mbalimbali kuanzia ngazi za Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa

Akifungua kikao kazi cha wadau kwa ajili ya kutoa maoni juu ya mkataba wa huduma kwa mteja wa Ofisi ya Rais –TAMISEMI leo Jijini Dodoma Bw.Kategere amefafanua kuwa mkataba huo umelenga katika kuhakikisha huduma bora zinatolewa kuanzia ngazi ya Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata, Tarafa, Vijiji na Vitongoji.

Ameendelea kusema kuwa kumekuwepo na mabadiliko mbalimbali yaliyojitokeza katika ngazi mbalimbali ikiwemo masuala ya utawala , utendaji kazi , mabadiliko ya maeneo ya kiutawala , teknolojia na mahitaji ya wadau , hivyo kuboresha mkataba huo, kutasaidia utoaji wa huduma zinazolingana na Mazingira ya sasa.

Amesema uwepo wa Mkataba wa Huduma kwa wateja kutasaidia kuboresha , utendaji wa kila siku ukiwemo mabadiliko ynayojitokeza katika utendaji kazi wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.

Kategere amesema kuwa madhumuni ya kuwepo kwa Mkataba wa Huduma kwa Mteja ni kuhakikisha wateja na wadau mbalimbali wanaelewa huduma zinazotolewa , viwango vya utoaji wa huduma, wajibu na haki waliyonayo wanapopatiwa huduma na utoaji wa maoni baada ya kupatiwa huduma.

Amewataka Wadau wanaopitia Rasimu ya Mkataba huo kuhakikisha wanaijadili kwa kina na kutoa maoni ambayo yatasaidia katika kuhakikisha wananchi na wadau mbalimbali wanapata huduma bora kwa wakati ili kupunguza malalamiko ambayo yamekuwa yakijitokeza katika suala zima la utoaji wa hudum kwa jamii.

Aidha ameishukuru Mradi wa Uimarishaji wa Mifumo ya Sekta za Umma PS3 Plus kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kufanya mapitio ya Mkataba wa Huduma wa mteja ambao umedhamiria kufanya maboresho ya mkataba ya Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa

Makataba wa Huduma kwa Mteja wa Ofisi ya Rais- TAMISEMI uliandaliwa mwaka 2010

No comments