RAIS SAMIA; LENGO LANGU NI KUIMARISHA USHIRIKIANO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, jana tarehe 02 Agosti, 2021 ameanza ziara Rasmi ya Kiserikali ya siku mbili nchini Rwanda kwa mwaliko wa Rais wa nchi hiyo Mhe. Paul Kagame.
Katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kigali, Mhe. Rais Samia amepokelewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Mhe. Vicent Biruta.
Mhe. Rais Samia amekagua gwaride la heshima lililoandaliwa kwa ajili yake na kufanya mazungumzo ya faragha na baadae kufanya mazungumzo rasmi na mwenyeji wake Rais wa Rwanda Mhe. Paul Kagame.
Mara baada ya mazungumzo hayo, Marais hao wawili wameshuhudia utiaji saini wa hati nne (4) za makubaliano ambazo zinahusu ushirikiano katika masuala ya Uhamiaji, Elimu, Teknolojia ya Habari na Mawasilinao, na Sheria ya Bidhaa za
Dawa.
Akizungumza wa waandishi wa habari, Mhe. Rais Samia amesema ziara yake nchini humo ina lengo la kuimarisha na kukuza ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Rwanda.
Aidha, Mhe. Rais Samia ametoa pole kwa Rais Kagame na wananchi wa Rwanda kwa tetemeko la ardhi lililoikumba nchi hiyo mwezi Mei mwaka 2021 na kusababisha madhara.
Vilevile, Mhe. Rais Samia ametembelea eneo la Gisozi Mjini Kigali, yalipo Makumbusho ya Mauaji ya kimbari na kuweka shada la maua na baadae kusaini kitabu cha wageni katika makumbusho hayo.
Post a Comment