WADAU WASHAURIWA KUWEKEZA KWENYE RASILIMALI WATU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Ummy Mwalimu (Mb) amewataka wadau wa maendeleo nchini kuwekeza katika Rasilimali watu ili kupata watumishi wenye weledi katika kutoa huduma bora ya afya kwa jamii.

Waziri Ummy ametoa wito huo leo Mkoani Kigoma mara baada ya kupokea vifaa tiba katika Hospitali,ya Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.

Alisisitiza kuwa kwa sasa kipaumbele cha Serikali ni miradi inayogusa maisha ya wananchi hasa katika seka za afya, miundombunu, elimu na maji katika ngazi ya msingi.

“Tunawasihi wadau wote wa maendeleo nchini kuelekeza nguvu zao katika kuwekeza kwenye miradi inayowalenga moja kwa moja wananchi badala ya kutenga bajeti kubwa kwa ajili mafunzo na semina,” alisema Ummy.

Waziri Ummy alieleza kuwa wadau wengi wa afya wamekuwa wakiwekeza sana katika semina na mikutano na kusahau kuwa vifaa vinavyoletwa kwa ajili ya kutolea huduma vinahitaji kuwa na wataalam ambao wanauwezo wa kuvitumia.

Aliwataka viongozi wa Mikoa, Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kuhakikisha wanapokaa na wadau wa maendeleo wahakikishe wanatoa vipaombele vitakavyosaidia kuleta mabadiliko katika sekta ya afya na elimu nchini.

Waziri Ummy amelipongeza shirika la “Medical Teams International Tanzania” kwa kutoa vifaa vyenye thamani ya shilingi miloni 335, ambavyo ni mashine ya mionzi (Xray), Ultsound na incubator kwa ajili ya Hospitali ya Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma.

Aidha, ameishukuru benki ya maendeleo Tanzania kwa kuunga mkono juhudi za Serikali za kuimarisha huduma za afya ya msingi kwa kutoa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni 12.

No comments