RAIS SAMIA ATOA POLE KWA WAFANYABIASHARA KARIAKOO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 11 Julai, 2021 ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Amos Makalla na Wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo kufuatia hasara kubwa waliyoipata kutokana na kuungua moto kwa Soko 

Kuu la Kariakoo lililopo Jijini Dar es Salaam.
Kufuatia hasara kubwa iliyotokana na kuungua kwa Soko hilo usiku wa Julai 10, 2021, Mhe. Rais Samia ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kufanya uchunguzi wa kina kujua chanzo cha moto huo.

Amesema Soko kuu la Kariakoo ni soko kubwa Jijini Dar es salaam ambalo lina mkusanyiko mkubwa wa wafanyabiashara na kuteketea kwa
soko hilo kutakuwa kumesababisha hasara kubwa kwa wapangaji na wamiliki wa soko hilo kongwe nchini. 

Mhe. Rais Samia amesema Soko la Kariakoo licha ya kuajiri wafanyabiashara wengi lakini ni kitovu cha biashara kwa nchi za Afrika Mashariki hivyo tukio hilo si hasara kwa Wafanyabiashara tu bali hata kwa Serikali.

Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia ametoa pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Mhe. Martin Shigella na Jumuiya za Kiislaam Tanzania
kufuatia kuungua moto kwa Bweni la Shule ya Sekondari ya Kiislam ya Wasichana AT TOWN inayomilikiwa na Taasisi ya Kiislam iliyopo
mji Mpya katika Manispaa ya Morogoro.

Mhe. Rais Samia amesema kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya kuungua moto kwa shule zinazomilikiwa na Jumuiya za Dini nchini hivyo ameviagiza vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kushirikiana na Jumuiya hizo kutafuta vyanzo vya matukio hayo na kuyadhibiti ili matukio
kuungua moto kwa shule hizo yasijirudie.


No comments