TAMKO LA KATAZO LA MISONGAMANO ISIYOKUWA YA LAZIMA

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA WAZEE NA WATOTO MHE DKT. DOROTHY GWAJIMA;-

"Kama tunavyofahamu Tanzania iko kwenye mapambano ya kudhibiti maambukizi ya UVIKO-19 ikiwa ni wimbi la 3 la mlipuko huu tangu uingie nchini Machi, 2020 Itakumbukwa kuwa Wizara ya Afya na Viongozi wa Serikali kwa ujumla wake kwenye ngazi mbalimbali wamekuwa wakitoa taarifa, elimu na kuhamasisha juu ya kujikinga na kuwakinga wengine dhidi ya maambukizi ya UVIKO-19"

"Serikali inatambua kuwa wananchi walio wengi wamekuwa wasikivu, wakiitikia na kutekeleza miongozo yote ya kujikinga na kuwakinga wengine ingawa kwenye baadhi ya maeneo mwitikio umekuwa siyo wa kuridhisha. Hali hii imeendelea kuchangia kuongezeka kwa maambukizi na hatimaye kuongezeka kwa idadi ya wagonjwa waliolazwa ambapo kufikia tarehe 21/07/2021 katika vituo vya huduma za afya kote nchini kulikuwa na wagonjwa 682 waliokuwa wanaugua maradhi ya UVIKO-19"

"Aidha, watalaamu wa afya wameendelea kupambana kwa moyo mmoja kuhakikisha huduma bora zinatolewa kwa wakati lakini hata hivyo baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakipoteza maisha"

"Ndugu Wananchi Wizara itaendelea kutoa takwimu hizi ili kwa pamoja tuendelee kufuatilia
hali halisi ya mwenendo wa ugonjwa huu huku tukiendelea kuchukua hatua za kutosha"

"Aidha, ili kuimarisha zaidi kasi ya kupambana na kudhibiti maambukizi ya UVIKO-19 natamka
kuwa, kuanzia leo tarehe 22/07/2021 nimekataza shughuli zote za misongamano yote isiyo ya lazima na ile yenye ulazima tahadhari ya kutosha ichukuliwe bila kuathiri shughuli za kiuchumi na kitaifa"

"Naelekeza Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuwapa ushirikiano Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Afya ya Jamii Na. 1 ya Mwaka 2009 na kuweka utaratibu mzuri kwa wale wanaoomba vibali vya shughuli zenye ulazima"

"Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wake wote itaendelea kutoa elimu na kufanya ufuatiliaji wa utekelezaji wa miongozo yote ya afya. Aidha, natoa wito kwa wananchi wote kujiandaa kupata huduma ya Chanjo kama ambavyo Mheshimiwa Waziri Mkuu alivyotoa taarifa jana tarehe 21/07/2021"

"Leo hii wataalamu wa afya wamekutana kupata mafunzo tayari kwa ajili ya kuwezesha upatikanaji wa huduma ya Chanjo dhidi ya UVIKO-19 kwa hiari na bila malipo"

"Taarifa zaidi zitaendelea kutolewa.
Wito wangu tuendelee kushikamana kwenye mapambano ya kutokomeza kabisa adui UVIKO-19 kwa kuzingatia utekelezaji wa afua zote za kujikinga na kuwakinga wengine zikiwemo;

1. Kuhakikisha sehemu zote zinazotoa huduma za kijamii zinakuwa na miundombinu ya huduma ya kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni na kama maji hakuna kuwe na matumizi ya vitakasa mikono.

2. Wananchi wote wanaotoa huduma za kijamii na wanaofika kupata huduma za kijamii wahakikishe wamezingatia afua za kinga zikiwemo kuvaa barakoa safi na salama.

3. Kwenye maeneo ya huduma za kijamii zinazokutanisha watu kadhaa kupata huduma
kanuni ya kuepuka misongamano izingatiwe kwa kuchukua tahadhari zote.

4. Kwenye vyombo vya usafiri utaratibu wa kuepuka kubeba abiria kwa kusongamana uzingatiwe na kabla abiria hao hawajaingia kwenye chombo husika kuwe na utaratibu wa kuhakikisha wamezingatia tahadhari zote za kujikinga na kuwakinga wengine.

5. Vilevile, nawakumbusha Wananchi tuendelee kuzingatia lishe bora, kufanya mazoezi na kutumia tiba asili zilizosajiliwa na baraza la tiba asili pasipo kuchelewa kufika kwenye vituo vya huduma kwa ushauri wa kitaalamu.

"Aidha, natoa wito kwa viongozi wa serikali na wa sekta binafsi na taasisi zake zote kuonesha
mfano kwa wananchi jinsi ambavyo wao wanatekeleza maagizo ya kuchukua tahadhari za
kinga dhidi ya Ugonjwa wa COVID-19. Vilevile, natoa wito wananchi kujiepusha na taarifa
zozote kuhusu UVIKO-19 kupitia watoa taarifa wasio rasmi."---- DOROTHY GWAJIMA

No comments