RUVU WAPEWA ONYO KALI, YANGA SC KULIPA FAINI MILIONI 3

KAMATI ya Uendeshaji na Usimamizi wa Ligi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) katika kikao chake cha Julai 6, 2021 ilipitia mwenendo na matukio mbalimbali ya Ligi Kuu na kufanya maamuzi yafuatao;

Ligi Kuu ya Vodacom 
Mechi Namba 287: Ruvu Shooting FC 1-1 Polisi Tanzania FC

Timu ya Ruvu Shooting FC imepewa onyo kali kwa kosa la mchezaji wa timu hiyo Samson Kwakwala kuvaa jezi yenye namba 71 mngongoni.

Kamati inazikumbusha klabu zote kuwa namba zinazoruhusiwa ni kati ya namba (Moja) hadi 60(Sitini) tu.

Tukio hilo lilitokea katika mchezo uliochezwa Juni 24, 2021 kwenye uwanja wa Mabatini mkoani Pwani.

Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 15(2.5) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za Mchezo.

Mechi Namba 208: Simba SC 0-1 Young Africans SC

Timu ya Young Africans SC imetozwa faini ya sh. 3,000,000 (milioni tatu) kwa makosa yafuatayo;
i) Kutumia mageti ya uwanja wa Uhuru kuingia uwanja wa Benjamin Mkapa badala ya mlango maalum unaotumiwa na timu.
ii) Kutumia mlango wa chumba cha waandishi wa habari (media center) badala ya mlango maalum unaotumiwa na timu.
iii) Kuingia uwanjani kupasha misuli (warm up) kwa kutumia mlango (Gate B) ambao haukupangwa kutumika kwa namna yoyote.
iv) Kutumia chumba cha wafanya usafi wa uwanja kwa ajili ya kubadilisha nguo badala ya chumba maalum cha kubadilishia nguo (Dressing Room).

Pia timu ya Young Africans SC inatakiwa kulipa Tsh. 850,000/= ikiwa ni gharama ya ukarabati wa mageti yaliyovunjwa wakati wa wakiingia uwanjani pamoja na makufuli ya uwanja wa Benjamin Mkapa yaliyoharibiwa katika tukio hilo.

Matukio hayo yalitokea katika mchezo uliochezwa Julai 3, 2021 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es Salaam.

Adhabu hii imetolewa kwa kuzingatia kanuni ya 15(15) ya Ligi Kuu kuhusu Taratibu za mchezo.

No comments