RAIS SAMIA AKUTANA NA BI. JOYCE MSUYA IKULU-DODOMA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 09 Julai, 2021 amekutana na kufanya mazungumzo na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP Bi. Joyce Msuya Ikulu Jijini Dodoma.

Bi. Msuya amesema UNEP kwa kushirikiana na Umoja wa Mataifa (UN) wako tayari kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika maendeleo na mipango yake ya kutunza na kuhifadhi mazingira.

Pia Naibu Mkurugenzi huyo wa UNEP ametoa salamu za pongezi kutoka kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Mhe. António Guterres na Naibu Katibu Mkuu Balozi Amina Mohammed kwa Mhe. Rais Samia kwa uongozi wake mahiri tangu ashike nafasi ya Urais nchini Tanzania.

Aidha, Bi Msuya amempongeza Mhe. Rais Samia kwa jitihada zake anazochukua kukabiliana na ugonjwa wa Corona ambapo amesema Umoja wa mataifa uko tayari kuunga mkono jitihada hizo.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi. Christine Musisi amesema kupitia mpango mkakati wa miaka mitano wanaouandaa utazingatia mpango wa maendeleo wa tatu wa miaka mitano (FYDP III) wa Tanzania.

Kwa upande wake Mhe. Rais Samia ameshukuru na kuahidi kuendelea kushirikiana na UNEP katika mipango thabiti ya utunzaji na uhifadhi wa mazingira nchini.

Mhe. Samia amewataka UN kuhakikisha kuwa mpango wao wa miaka mitano wanaouandaa uwe endelevu na wenye kuleta tija katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Pia, Mhe. Samia amesema Serikali inaendelea na jitihada mbalimbali za kukabiliana na uharibifu wa mazingira ikiwa ni pamoja na kuwawekea mazingira bora wananchi katika shughuli zao za maendeleo ili wasizidi kuharibu mazingira.

Mhe. Rais amewaomba UNEP kwa kushirikiana na UN kuendeleza jitihada za Serikali kwa kuwapatia rasilimali fedha na rasilimali watu ili
azma ya kutunza mazingira ifanikiwe kikamilifu.

No comments