PROF. MAKUBI; WANAOINGIA HOSPITALI WAPIMWE JOTO

"kwenye maeneo ya kutolea huduma za Afya, kwenye mahospitali na sehemu nyingine miundombinu ya kunawia mikono iwekwe pia tanapowezekana watu wapimwe joto pindi kabla ya kuingia, na walio na uwezo watumie vipukusi (sanitizers) hususan wagonjwa au ndugu wanapofika kwenye wodi" Prof. Abel Makubi, Katibu Mkuu Wizara ya Afya wakati akitoa mwongozo wa kudhibiti ugonjwa wa Corona bila kuathiri shughuli za kiuchumi mbele ya Waandishi wa habari katika ofisi ndogo za Wizara ya Afya Jijini Dar es Salaam.

Pia, ameagiza idadi ya watu au ndugu wanaokwenda kusalimia wagonjwa ipunguzwe, huku akisisitiza wasizidi wawili kwa wakati mmoja.

Aidha, amepiga marufuku kwa walinzi wa mageti ya Hospitali kutumia nguvu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona na kusisitiza elimu itolewe kwa wahitaji wa kuona wagonjwa pindi watapoenda kinyume na hatua za kinga dhidi ya ugonjwa wa Corona.

Hata hivyo, ametoa wito kwa vyombo vya usafiri kuweka matangazo ya elimu ya kujikinga dhidi ya ugonjwa wa Corona katika tv na redio ili abilia wapate elimu hiyo itayosaidia katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

Kwa upande mwingine amewataka wananchi wanokwenda kupata huduma katika mahakama na polisi kuhakikisha wanavaa Barakoa muda wote, huku akitoa wito kwa Watoa huduma katika maeneo hayo kuhakikisha wanaweka vyombo vya kunawia mikono na sabuni ili kuvunja mnyororo wa maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Mbali na hayo amewataka wamiliki wa saluni za kike na kiume kuwa na vifaa vya kutosha vya kunawia mikono, huku akisisitiza usafi wa taulo za kuwahudumia wateja zikiwa zimefuliwa na kupigwa pasi kabla ya kuitumia kwa mteja mwingine.

No comments