MARAIS, MAWAZIRI WAPONGEZA KASI YA MRADI WA JNHPP

Marais Wastaafu, Mhe. Ali Hassan Mwinyi na Mhe. Jakaya Kikwete wakiambatana na Mawaziri Wakuu wastaafu Mhe. Cleopa Msuya, Mhe. John Malechela pamoja na Mhe. Mizengo Pinda leo Julai 05, 2021 wametembelea mradi wa kufua umeme kwa njia ya maji wa megawati 2115 wa Julius Nyerere, unaotekelezwa kwenye bonde la mto Rufiji na kupongeza kasi kubwa ya utekelezaji wa Mradi huo.

Katika ziara hiyo viongozi hao wakuu wameipongeza Serikali kwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa maradi na hasa kwa kuwaamini Watanzania katika usimamizi wa ujenzi wa mradi.

Akiwa katika mradi huo Rais mstaafu Mhe. Ali Hassan Mwinyi amesema kuwa, Taifa linajivunia ujenzi wa mradi na kusistiza kuwa, vizazi vya sasa vina kila sababu kujivunia mradi huo kwani utafungua fursa nyingi za kimaendeleo.

“Vijana wetu wanatakiwa kujivunia mradi huu kwani sisi sasa ni wazee hivyo manufaa makubwa ya mradi huu ni vijana wa sasa utawasaidia sana kuwa na maendeleo, hivyo cha msingi ni kuongeza bidii katika elimu” alisema Mhe. Mwinyi

Kwa upande wake, Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Mhe. Jakaya M. Kikwete, aliipongeza Serikali ya awamu ya tano iliyokuwa chini ya Hayati Dkt. John Magufuli kwa kuonesha udhubutu wake kwa kuanzisha ujenzi wa mradi huo ambapo alishauri Wizara ya Nishati kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji kwa fursa zitakazo ambatana na kukamilika kwa bwawa hilo.

Dkt. Jakaya Kikwete alisema kuwa, mradi wa Julius Nyerere utakapokamilika utakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa sambamba na kuchochea ukuwaji wa uchumi wa Taifa zima kwa ujumla.

 “Nina uhakika  Rais Samia Suhulu Hassan, atahakikisha mradi huu unakwenda sambamba na matarajio ya mtangulizi wake na kukamilika kwa wakati" alisema Dkt. Kikwete.

Aliongeza kuwa, wananchi wa Mikoa kumi na moja, iliyo na vyanzo vya maji ya mto Rufiji ambao unategemewa sana katika bwawa la Nyerere kuvilinda vyanzo hivyo kwani bila kuvilinda mradi huo hautaleta tija.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Mstaafu, Mhe. Mizengo Pinda amepongeza Wahandisi wazawa kwa usimamizi wa mradi, ambao uliasisiwa na Serikali ya awamu ya kwanza na kutekelezwa na Serikali ya awamu ya tano.

No comments