HII HAPA SHERIA YA CHAKULA KATIKA BIBLIA
*_SHERIA YA CHAKULA_*
*UTANGULIZI*
Chakula ambacho mwanadamu anapaswa kula kimeandikwa
katika Maandiko, na ni moja kati ya sheria za Mungu. Bahati
mbaya somo hili halieleweki vizuri na linafundishwa tofauti na
inavyotakiwa kuwa.
*Hebu fuatilia historia hii ya kipekee ya maagizo ya Mungu juu ya chakula.*
*Chakula Kabla ya Dhambi:* Matunda Yenye Mbegu Ndani
Chakula ilikuwa ni moja ya mada za hotuba ya kwanza kabisa
ya Mungu baada ya kumwumba mwanadamu. Katika wiki ya
kwanza ya uumbaji Mungu alitoa mwongozo juu ya chakula
kwa wazazi wetu wa mwanzo akisema;
*_“… Tazama, nimewapa kila mche utoao mbegu … na kila mti, ambao matunda yake yana mbegu; vitakuwa ndivyo chakula chenu …” Mwanzo 1:29._*
*Chakula Baada ya Dhambi:* *Vyakula Aina Ya Mboga-mboga*
Baada ya dhambi kuingia Mungu aliwaongezea wanadamu
vyakula aina ya mboga mboga katika orodha za chakula
ambavyo walipaswa kula.
Mwanzo 3:17-18 imeandikwa;
*_“Akamwambia Adamu … nawe utakula mboga za kondeni”_*
*Chakula Baada ya Gharika:*
Kwa sababu ya kutokuwepo kwa vyakula juu ya nchi mara tu
baada ya gharika, Mungu aliwaruhusu wanadamu kuanza kula
nyama za wanyama walio safi. Kumbuka kuwa hata kabla ya
kuwaruhusu wanadamu kula nyama, Mungu alikuwa
ametenganisha wanyama najisi na safi.
Kabla ya gharika Mungu alimwagiza Nuhu aingize ndani ya safina, jozi za
wanyama kulingana na kwamba ni safi au najisi.
Mwanzo 7:2-
3 inasema;
*_“Katika wanyama wote walio safi ujitwalie saba saba, mume na mke; na katika wanyama wasio safi wawili wawili, mume na mke.”_*
*Maagizo Yaandikwa Rasmi Katika Chuo:*
Karne nyingi baadaye baada ya gharika ya Nuhu, Mungu
alimwagiza nabii Musa kuandika sheria hii katika kitabu cha
sheria (torati).
Hizi ndizo aina za vyakula vinavyofaa na vile
visivyofaa kulingana na sheria hii.
*👉🏾1. Wanyama wafaao kuliwa Walawi 11:2,3:* *Wanyama safi na halali kuliwa ni hawa:*
*_"Kila mwenye kwato katika miguu yake, mwenye miguu ya kupasuka kati, mwenye kucheua, … hao ndio mtakaowala" Kumbukumbu 14:7-8:_*
*Wanyama najisi na machukizo:*
*_"ngamia, sungura, nguruwe n.k"_*
*👉🏾2. Samaki wafaao kuliwa Walawi 11:9-10* samaki walio halali kuliwa na watu wa
Mungu ni *_"Kila aliye na mapezi na magamba"._*
Samaki najisi
na machukizo wasiofaa kuliwa na watu wa Mungu ni *_"wote wasio na mapezi na magamba"._*
*Hii ni sawa na kusema kuwa samaki aina ya kambale na wale wote wasiokuwa na sifa hizi hawafai kuhesabiwa kuwa chakula katika jamii ya watu wa Mungu.*
*👉🏾3. Ndege wasiofaa ni wale wote walao mizoga*
*👉🏾4. Pombe, Sigara na Madawa ya Kulevya:*
Aina nyingine ya vitu visivyofaa kuingizwa katika miili ya
watu wa Mungu ni kama vile pombe, sigara na madawa ya
kulevya. Vitu vyote vinavyoudhuru mwili havifai kutumiwa kwa kiwango chochote.
*Mtu yeyote asiseme kuwa mimi natumia kiasi kidogo tu.* Haramu ni haramu, najisi ni najisi,
ikiwa ni kwa kiwango kidogo au kikubwa, ni najisi tu,
usitumie.
Katika habari ya pombe maandiko yanasema;
*_“Mvinyo hudhihaki, kileo huleta ugomvi; Na akosaye kwa vitu hivyo hana hekima.” Mithali 20:1_*
*AGANO JIPYA NA CHAKULA:*
Watu wengi wanadai kuwa Yesu alihalalisha kula kila kitu pale
Maandiko yanaposema;
*_“… Kwa kusema hivi alivitakasa vyakula vyote.” Marko 7:19_*
*Hapa ndipo usomaji makini unapohitajika ili kuelewa vizuri ujumbe ulioandikwa. Usomaji makini wa Maandiko unaonesha kuwa:*
*👉🏾(1) Katika Israeli kila kinachoitwa chakula kilikuwa
kimeainishwa kama tulivyonukuu hapo juu. Kila kitu
ambacho hakikuorodheshwa kwenye orodha hiyo
hakikuitwa chakula. Kwa hiyo maandiko matakatifu
yanaposema kuwa Yesu alivitakasa vyakula vyote maana
yake alitasa vile ambavyo vilijulikana kuwa ni vyakula tu. *Hata hivyo, ikumbukwe kuwa hoja ya msingi ilikuwa ni wanafunzi kula chakula bila kunawa mikono.*
*👉🏾(2) Mada iliyokuwa inaongelewa katika sura hii haikuwa aina ya vyakula bali utaratibu wa kunawa kabla ya kula.* Wakati
ule kulikuwa na mafundisho (mapokeo tu) ya mafarisayo
kuwa mtu asiponawa mpaka kwenye kiwiko anakuwa
amekitia chakula hicho unajisi kwa mikono najisi.
*Hili halikuwa fundisho la Mungu.* Juu ya hili Maandiko katika
Marko 7:2-3 yanasema;
*_“Kisha Mafarisayo, na baadhi ya waandishi waliotoka Yerusalemu, wakakusanyika mbele yake, wakaona wengine katika wanafunzi wake wakila vyakula kwa mikono najisi, yaani, isiyonawiwa. Kwa maana Mafarisayo na Wayahudi wote wasiponawa mikono mpaka kiwiko, hawali, wakishika mapokeo ya wazee wao."_*
👉🏾Kisa kingine kinachotatanisha wengi ni cha maono ya Petro ya
kitambaa kilichokuwa na viumbe najisi na kauli toka mbinguni
ikimwambia kuwa achinje na ale, na alipokataa akaambiwa
alichokiumba Mungu asikiite najisi (Matendo 10:1-28).
*_“ … Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba … akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia, akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi; ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani. Kisha sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule. Lakini Petro akasema, Hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi. Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi. … Hata Petro alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuiulizia nyumba ya Simoni, wakasimama mbele ya mlango, wakaita; wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro anakaa humo. Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta. Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma ... Petro akaondoka akatoka pamoja nao, …Akawaambia, Ninyi mnajua ya kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa taifa lingine wala kumwendea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu awaye yote mchafu wala najisi.”_*
*👉🏾Usomaji makini juu ya maono unaonesha kuwa:*
(1) Maono haya yalitokea baada ya Yesu kupaa mbinguni.
Kwa hiyo kama Yesu alikuwa ameruhusu kula kila kitu kabla
ya kupaa, Petro asingeliendelea kuviita vitu hivyo najisi.
Matendo 10: 10 *_“Lakini Petro akasema, Hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi.”_*
Aya hizi zinaonesha kuwa Petro hakuwahi kula vyakula najisi
kwa kipindi cha maisha yake yote. Kama Yesu angelikuwa
amehalalisha kula kila kitu Petro asingeendelea kuwa na
msimamo huo wa kukataa katika hayo maono. Hii ni kwa
kuwa Petro alikuwa na Yesu kwa zaidi ya miaka mitatu, kwa
kipindi hicho angelikuwa anajua kuwa Mungu
ameshavihalalisha vitu hivyo na hivyo yeye alikuwa hana
mamlaka ya kusema kuwa ni najisi.
*(2) Maono haya hayakuhusu aina za vyakula bali aina ya watu.* Wakati ule wayahudi waliwaita mataifa mengine kuwa
ni najisi. Hivyo kauli iliyotolewa kuwa alichokiumba Mungu
asikiite najisi ilikuwa na maana kuwa asiwaite watu wasio
Wayahudi kuwa ni najisi.
Petro mwenyewe alifafanua maono
yake katika Matendo 10:28 akisema;
*_“… Ninyi mnajua ya kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa taifa lingine wala kumwendea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu awaye yote mchafu wala najisi."_*
*HITIMISHO:*
Wanadamu wamepewa aina za vyakula vinavyofaa kwa
chakula. Maandiko yanasisitiza juu ya sheria hii yakisema;
*_“Basi, mlapo, au mnywapo, fanyeni yote kwa utukufu wa Mungu.” 1 Wakorintho 10:31._*
*Hakuna mahali katika Maandiko ambapo Mungu ameruhusu kula kila kitu. Mungu ametoa maelekezo juu kile tunachopaswa na tusichopaswa kula.*
*_Anasema angalieni msijitie unajisi kwa kula vitu hivyo; takaseni nafsi zenu, iweni watakatifu kama vile baba yenu wa mbinguni alivyo mtakatifu (Walawi 11:44)._*
*Kumbuka ulimwengu huu ulianguka katika dhambi kwa kuvunja amri juu ya chakula.*
*Yesu pia alijaribiwa juu ya chakula lakini Yeye akashinda. Wewe nawe kadhalika Shetani anakujaribu juu ya vyakula, ule najisi - angalia ukatii sauti ya Mungu nawe utaishi._*
*Mungu akubariki sana unapotafakari somo hili na kufanya uamuzi kulingana na maandiko.*
Barikiwa,kwa ufafanuzi mzuri.
ReplyDelete