AIFELLO ASEMA KANSA IKIGUNDULIKA MAPEMA INATIBIKA

Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Aifello Sichalwe ameweka wazi kuwa ugonjwa wa Saratani unaweza kutibika endapo mgonjwa ataanza kupata matibabu mapema baada ya kugundulika ana ugonjwa huo.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizindua kitabu cha "ujue ugonjwa wa Saratani " kilichoandikwa na Dkt. Hellen Makwani na kuzinduliwa tarehe 2 Julai 2021 na Mganga Mkuu wa Serikali Jijini Dar es Salaam.

"Lengo la shughuli hii ni kuisaidia jamii kuelewa vihatarishi vya Saratani, dalili na njia za ugunduzi wa Saratani katika hatua ya awali ili watu waweze kuchukua hatua mapema iwezekanavyo kwani Saratani hupona ikigundulika katika hatua za awali" amesema Dkt. Aifello Sichalwe.

Aliendelea kusema kuwa, utolewaji wa elimu kwa Jamii juu ya ugunduzi wa Saratani katika hatua za awali ni sehemu ya Mkakati wa Kitaifa wa kudhibiti ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa Saratani.

Hata hivyo Dkt. Sichalwe ameagiza kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa Saratani kwa kuelimisha juu ya ulaji unaofaa, umuhimu wa ufanyaji mazoezi, kuelimisha juu ya madhara ya matumizi ya pombe kupita kiasi na tumbaku.

Aidha, Dkt. Sichalwe ameweka wazi kuwa, takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Tafiti za Saratani (IARC) za 2018 zinaonesha wagonjwa 76 wa Saratani kwa kila watu 100,000 hubainika kila mwaka, hii ni sawa na makadirio ya wagonjwa wapya wa Saratani 42,060 kwa mwaka huku taarifa za vifo zikibainisha takribani wagonjwa 28,610 hufariki kwa mwaka ambapo 68% ya waliofariki ni wagonjwa wapya.

Naye Muasisi wa Taasisi ya Genesis na Mwandishi wa Kitabu cha Ijue Saratani Dkt. Hellen Makwani amesema kuwa, lengo la taasisi hiyo ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 elimu ya utambuzi mapema iwe inasaidia kutambua Saratani hatua za awali na ikiwezekana kuwe na matokeo ya asilimia 75 ya watu wagundulike katika hatua za awali za ugonjwa huo.

"Lengo la taasisi hii, ni kuhakikisha ifikapo 2030 elimu ya utambuzi mapema iwe inasaidia kutambua Saratani hatua za awali na ikiwezekana tuweze kuwa na matokeo ya asilimia 75 wagundulike hatua za awali kinyume na ilivyo sasa" amesema Dkt. Hellen Makwani.

No comments