ZIARA YA KUSHTUKIZA KIWANDA CHA H&J LIMITED

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo amefanya ziara ya kushtukizia katika kiwanda cha H & J Limited kinachozalisha mifuko ya viroba kilichopo Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani. 

Jafo akiwa kwenye ziara ya ukaguzi wa Mazingira katika kiwanda hicho amebaini changamoto mbalimbali za kimazingira ikiwemo utiririshwaji wa maji machafu kutoka kiwandani hapo na kwenda kwenye Mto Mbiki uliopo karibu na kiwanda hicho.

Amesema changamoto nyingine ni uchomaji wa mifuko inayotumia malighafi ya plastiki pamoja na wafanyakazi wa kiwanda hicho kutokuwa na vifaa vya kufanyia kazi.

Aidha amewataka wenye kiwanda hicho kurekebisha mara moja changamoto hizo ili kuepusha uchafuzi wa mazingira. Ameendellea kusema kuwa hayupo tayari kukifumbia macho kiwanda chochote kitakachohusika na uchafuzi wa mazingira kwani Serikali inataka maendeleo yenye tija na yanayohifadhi mazingira

“Sijaridhika na kiwanda hiki kinavyoendeshwa kwani kinachangamoto nyingi ikiwemo utiririshwaji wa maji kutoka kiwandani na kwenda kwenye mto mbiki, hivyo niwatake @nemctanzania kuja hapa na kufanya ukaguzi pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria ya mazingira. Pia natoa miezi sita kwa kiwanda hiki kuweka mfumo wa uchujaji maji yanayotoka kiwandani kabla ya kwenda kwenye mazingira” Jafo alisema

Meneja wa Kanda ya Mashariki Kaskazini Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Anorld Mapinduzi, amesema kuwa kiwanda cha H& J kilisajiliwa kwa ajili ya kupata cheti cha mazingira lakini mchakato wa upatikanaji wa cheti haujakamilika na kiwanda kimeanza kufanya shughuli zake.

“Tumepokea maelekezo ya Waziri na tutakuja kufanya ukaguzi wa kina ili tuweze kuwachukulia hatua kulingana na sheria na kanuni ya Mazingira. Ikiwa NEMC imepewa mamlaka ya kusimamia mazingira hatupo tayari kuona wananchi wanaathirika kwa moshi, vumbi au kemikali zozote,” alisema.

Vile vile Mhe. Jafo amekagua kiwanda cha Keda Ceramic Limited kilichopo Halmashauri ya Chalinze Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani kinachojihusisha na uzalishaji wa marumaru, amekipongeza kiwanda hicho kwa jinsi wanavyofanya shughuli zao bila kuathiriri mazingira

No comments