WIZARA YA HABARI YAVUKA LENGO

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imevuka lengo la ukusanyaji mapato kwa kukusanya jumla ya kiasi cha Sh.1, 080,109,491 ambazo ni sawa na asilimia 113 hadi kufikia Mei, 2021 kutoka Sh. 960,000,000/= kiasi ambacho kilikadiriwa kukusanywa kwa mwaka 2020/21.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa alipowasilisha Bungeni Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2021/2022.

Mafanikio ya makusanyo hayo yanatokana na usimamizi wa makusanyo ya Serikali kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali ya nchi na kuongezeka kwa utoaji wa huduma zinazotolewa na Wizara katika sekta za Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Kuhusu sekta ya Habari, Waziri Bashungwa amesema “Wigo wa vyombo vya habari umeendelea kuongezwa nchini ili kuhakikisha wananchi wanapata haki yao ya kikatiba ya kupata taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu kwa maisha na shughuli zao”.

Hadi kufikia mwezi Mei 2021 ina idadi ya magazeti na majarida yaliyosajiliwa 257; vituo vya televisheni 43, vituo vya redio 200, televisheni mtandao 451, redio mtandao 23, blogu 122 na jukwaa mtandaoni ni 09 hatua inayoonesha namna nchi inavyoendelea kurahisisha na kuimarisha uhuru wa upatikanaji wa habari kwa wananchi.

Katika kuimarisha usikivu wa Redio za TBC,, Serikali imeendelea kuongeza usikivu wa redio kutoka Wilaya 87 mwaka 2017 hadi Wilaya 102 mwaka 2021.

Miradi inayoendelea kutekelezwa kwa ajili ya kuongeza mawanda na usikivu katika Wilaya za Ngara, Kyela, Ruangwa, Kilombero na Ludewa ujenzi wa mitambo ya redio ya FM unaoendelea katika Wilaya za Tanganyika, Makete, Uvinza, Mbinga na Ngorongoro itasaidia kuongezeka kwa usikivu a kufikia Wilaya 119 kati ya Wilaya zote 161 sawa na asilimia 74 ambapo matarajio ya ni usikivu wa redio kuzifikia Wilaya 134 sawa na asilimia 83 za Tanzania Bara pamoja na visiwa vya unguja na Pemba kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022.

No comments