WANAFUNZI 17,000 KUSHIRIKI UMITASHUMTA, UMISSETA

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Prof. Riziki Shemdoe amesema kuwa Jumla ya wanafunzi kutoka 7,400 wanatarajiwa kushiriki Mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa shule za Msingi (UMITASHUMTA) na Umoja wa Michezo wa shule za Sekondari (UMISSETA) yatakayofanyika mkoani Mtwara.

Akizungumza na wanahabari  jijini Dodoma, Prof. Riziki Shemdoe amesema jumla ya washiriki 3,600 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara wanatarajiwa kushiriki mashindano ya UMITASHUMTA ambapo washiriki 3,800 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar watashiriki katika Michezo ya UMISSETA.

"Ufunguzi wa mashindano hayo utafanyika tarehe 08/06/2021 kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona uliopo katika Manispaa ya Mtwara ambapo Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa," amesema Prof.Shemdoe

Ameendelea kufafanua kuwa mashindano ya UMITASHUMTA yatafanyika kuanzia Juni 6 mpaka Juni 19, 2021 ambapo michezo ya UMISSETA itaanza Juni 19 hadi Julai 3, 2021.

Hata hivyo, Prof. Shemdoe ameitaja michezo itakayoshindaniwa kwa upande wa UMITASHUMTA ni pamoja na mpira wa miguu kwa wasichana na wavulana, mpira wa miguu maalum kwa wavulana wenye ulemavu wa kusikia, na netiboli.

Michezo mengine ni mpira wa goli kwa wasichana na wavulana wasioona na wenye uoni hafifu, mpira wa wavu kwa wasichana na wavulana, na mpira wa mikono kwa wasichana na wavulana.
Mengine ni mpira wa meza kwa wasichana na wavulana, riadha jumuishi, kwaya na ngoma.

Aidha, amesema awamu zote mbili zitahusisha mashindano ya usafi katika mazingira wanayoishi kwa ujumla wake pamoja na nidhamu yao wakiwa kambini na michezoni.

"Niwaalike Watanzania wote kuja Mtwara kushuhudia vijana wetu wakionesha vipaji na vipawa vyao katika michezo na sanaa," amesema Prof Shemdoe.

No comments