SHARTI LA KUVAA BARAKOA ENEO LA HOSPITALI YA MUHIMBILI

KUTOKA WIZARA YA AFYA;
Mtakumbuka kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeziagiza taasisi mbalimbali kuendelea kuchukua tahadhari ili kujikinga na kuwakinga wananchi dhidi ya ugonjwa wa COVID 19 na uwezekano wa kutokea wimbi la tatu la ugonjwa huu. 

Ili kutekeleza maagizo hayo, Uongozi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili unatoa maelekezo yafuatayo kwa wagonjwa, wafanyakazi, wanafunzi na wananchi wote wanaoingia eneo hilo (Upanga & Mloganzila) kuzingatia yafuatayo;

1. Kuvaa barakoa wakati wote wanapokua katika mazingira ya Hospitali. Hakuna atakayeruhusiwa kuingia ndani ya eneo la Hospitali bila kuvaa barakoa.

2. Wafanyakazi wote na wanafunzi kuanzia sasa wanapaswa kuvaa barakoa wakati wote wakiwa mazingira ya kazi. Hakuna mfanyakazi au mwanafunzi atakayeruhusiwa kutoa huduma kwa mgonjwa bila kuvaa barakoa kuanzia kliniki, kwenye vipimo, wodini nk

3. Aidha, tunawaelekeza wafanyakazi, wanafunzi ndugu na jamaa wa wagonjwa wote wanaoingia eneo la Hospitali kunawa mikono kwa kutumia sabuni na maji tiririka yaliyopo katika maeneo mbalimbali ya hospitali au vipukusi (sanitizer).

4. Eneo la Muhimbili lina msongamano, hivyo tunashauri idadi ya wasindikizaji kwa wagonjwa wanaokuja kliniki nayo kupungua hivyo mgonjwa ataruhusiwa kuja na msindikizaji mmoja.

5. Wagonjwa waliolazwa wodini wataruhusiwa kuonwa na ndugu zao watano tu kwa siku ambapo asubuhi ni ndugu wawili, mchana mmoja na jioni wawili.

6. Tunawaomba wananchi kuunga mkono hatua hizi ili kuongeza tahadhari za kujikinga
dhidi ya ugonjwa huu wa COVID 19. Utekelezaji wa maelekezo haya unaanza rasmi
tarehe 23 Juni, 2021.

No comments