SERIKALI YAANZA KUPOKEA MAONI YA WADAU

Serikali iko tayari kupokea maoni na mapendekezo yanayotolewa na wadau juu ya nini kifanyike ili kuboresha sheria na kanuni zinazounda Bodi ya Kitaalamu ya Walimu Tanzania.

Hayo yamesemwa Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako (Mb) wakati akifungua Kikao cha wadau kuhusu Bodi ya Kitaalamu ya Walimu ambapo amesema lengo ni kuhakikisha utekelezaji wa sheria na kanuni uweze kuleta tija pande zote.

Prof. Ndalichako amesema kuwa mwaka 2018 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha muswada wa sheria ya kuunda Bodi ya Kitaalamu ya Walimu ya Tanzania, ambapo Wizara ya Elimu ilitunga kanuni za kuwezesha utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo baada ya kusainiwa kwa sheria hiyo.

Kiongozi huyo amesema kuwa baada ya kutungwa kanuni hizo, Chama cha Walimu Tanzania kilielezea kutoridhishwa na baadhi ya vipengele vya kanuni hizo, hivyo Wizara imeona ni vema kuwashirikisha wadau na kuamua kuitisha kikao ambacho kitasikiliza maeneo ya Kanuni na Sheria za Bodi hiyo yanayoonekana yataleta changamoto katika utekelezaji.

No comments