SERIKALI YA AWAMU YA NANE IMEDHAMIRIA-HUSSEIN MWINYI
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ina dhamira ya dhati ya kupanua wigo wa matumizi endelevu ya bahari na rasilimali zake ili kujenga uchumi imara kwa Taifa.
Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo huko katika ukumbi wa Hoteli ya Verde nje kidogo ya Jijini la Zanzibar wakati akifungua Kongamano la siku moja lililobeba mada “Uchumi wa Buluu kwa Maendeleo ya Kijamii, Kiuchumi na Uhifadhi wa Mazingira Zanzibar”.
Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alieleza kuwa bado kuna fursa, faida na vipaumbele vya uwekezaji zaidi chini ya Uchumi wa Buluu kama vile katika sekta za uvuvi mdogo mdogo, uvuvi wa bahari kuu, ufugaji samaki na mazao ya bahari.
Alizitaja Sekta nyengine kuwa ni ukulima wa mwani, ujenzi wa miundombinu ya kimkakati ya usafiri baharini, zikiwemo bandari, viwanda vya kusindika samaki, uchimbaji wa mafuta na gesi, pamoja na shughuli za utalii wa fukwe na michezo ya baharini.
Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa maamuzi hayo ya uwekezaji zaidi katika uchumi wa bahari yamefanikiwa kwa kutambua uwezo na mchango wa maliasili na rasilimali za pwani na baharini zinazozunguka visiwa vidogo vidogo.
Aliongeza kuwa katika kuhamasisha matumizi endelevu ya bahari katika uzalishaji na upatikanaji wa ajira kwa Wazanzibari, Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha kwamba inafanikiwa katika kutekeleza azma hiyo.
Alisema kuwa sekta ya uvuvi ni muhimu kwa maendeleo ya Zanzibar lakini hata hivyo bado haijawanufaisha Wazanzibari wengi.
Hivyo, kupitia dhana hii ya uchumi wa Buluu, Serikali inafanya jitihada za dhati za kuendeleza uvuvi wa bahari kuu na tayari mipango ya kununua vyombo vitakavyotumika kwenye aina hii ya uvuvi imekamilika.
Post a Comment