MAJALIWA AKERWA MAAFISA UGANI KUKAA OFISINI

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa amekerwa na tabia ya maafisa ugani kukaa ofisini badala ya kwenda shambani kutembelea wakulima na kuwapatia elimu bora juu ya matumizi sahihi ya viuatilfu ili waweze kuzalsha kwa tija na kuongeza kipato.

Waziri Mkuu aliyasema hayo alipokuwa akizungumza katika kikao cha wadau wa tasnia ya korosho leo tarehe 6/6/2021 katika ukumbi wa Sea View Resort mjini Lindi.

“Maafisa kilimo kurundikana pale ofisini mtoke muende shambani, makao makuu tubaki na maafisa kilimo wawili afisa kilimo wa wilaya na afisa bustani.sekta ya kilimo ni field officers sio desk officers” alikaririwa akisema
Waziri Mkuu pia ametoa maagizo kwa Wizara ya Kilimo kuwa na idadi sahihi ya wakulima wanaolima zao la korosho,ukubwa wa shamba ili kujua mahitaji ya pembejeo katika msimu wa kilimo. 

Pia amesema kuwa korosho ni zao linaloingizia Taifa kipato kikubwa likiwa ni zao la kibiashara , mazao mengine ya kibiashara ni pamoja na pamba,tumbaku,chai na kahawa.

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa Serikali ya Awamu ya sita imeweka msisitizo katika kilimo na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ameagiza kila pembejeo ifike kwa mkulima kwa wakati kabla ya miezi miwili ya msimu na ametoa kibali cha kulipa wakulima fedha zao wanazodai.

Hata hivyo Waziri Mkuu amesisitiza kwa wakulima kutumia ushirika ili waweze kupata masoko ya mazao yao pamoja na mikopo kutoka benki kwa kuzingatia vikundi vya ushirika ili iwe rahisi kukopesheka.

Naye Waziri wa Kilimo Mhe.Adolf Mkenda amesema kuwa wakulima wakitumia pembejeo kikamilifu na kwa mfumo sahihi mti mmoja unaweza ukatoa kilo 35 za korosho na kusababisha nchi kutoka kwenye kilo 15 mpaka kilo 35 za korosho ongezeko hilo ni kubwa na lina tija lakini bado halijafikiwa kutokana na changamoto mbalimbali.

“Kama tungeweza kuongeza tija kwenye uzalishaji wa korosho kwa miti hii tuliyonayo na kufanya mabadiliko kidogo kwa baadhi ya miti tungeweza kuongeza mapato ya korosho kutoka bilioni 279.8 ambazo ndizo tunazipata kwa sasa hivi mpaka kufikia sh trilioni 1.971 kwa mwaka.”alisema Mkenda

No comments