AMKA NA BWANA LEO 2
KESHA LA ASUBUHI
JUMATANO, JUNI, 2, 2021
SOMO: BWANA WETU NI MKARIMU
Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali.
Mathayo 6:24.
Imeandikwa waziwazi kuhusu moyo ambao haujafanywa upya na kuhusu ulimwengu ulioanguka, wote wanatafuta yawapendezao. Ubinafsi ni kanuni kubwa ya asili yetu iliyoharibika. Ubinafsi unachukua nafasi kwenye roho ambapo Kristo anapaswa kuchukua nafasi. Lakini Bwana anahitaji utii mkamilifu, na kama kweli tunatamani kumtumikia, hakutakuwa na swali katika akili zetu kuhusu iwapo tunapaswa kutii matakwa Yake au kutafuta mambo yetu yasiyo ya kudumu.
Bwana wa utukufu hakufuata mambo aliyoona yanamfaa au yanayompendeza alipoondoka kwenye ofisi yake ya cheo cha juu na kuwa Mtu wa huzuni aliyezoea shida, akiikubali aibu na kifo ili amkomboe mwanadamu kutoka katika madhara ya kutokutii kwake. Yesu alikufa si kwa ajili ya kumwokoa mwanadamu katika dhambi zake, bali kumtoa dhambini. Tunapaswa kuacha makosa ya njia zetu, tuuchukue msalaba wetu na kumfuata Kristo, tukijikana nafsi, na kumtii Mungu kwa gharama yoyote.
Wale ambao wanasema wanamtumikia Mungu, lakini wanatumikia mali, watatembelewa na hukumu. Hakuna ambaye atahesabiwa haki kwa kutotii kwa sababu ya kupata faida za kiduni. Ikiwa Mungu atamwacha mtu mmoja, angeweza kuwaacha wote. Wale ambao hawazingatii amri Za wazi za Bwana kwa kufuata maslahi binafsi, wanajiletea hukumu katika siku zijazo. Kristo alisema: “Je! Haikuandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala kwa mataifa yote? Bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi.” (Marko 11:17). Watu wa Mungu wanapaswa kuchunguza kwa karibu, ikiwa hawajafanya nyumba ya Mungu kuwa sehemu ya biashara, kama Wayahudi wa zamani.
Wengi wanaanguka katika dhambi ya kuipoteza dini yao kwa kutafuta tena maslahi ya kidunia, wakionesha namna ya utaua, lakini akili yao yote wakiiweka katika mambo yapitayo ya dunia hii. Lakini sheria ya Mungu inapaswa kutafakariwa kabla ya yote, na kutiiwa katika roho na maneno. Yesu, mfano wetu mkubwa, katika maisha yake na kifo alifundisha utii mkamilifu. Alikufa, mwenye haki kwa wasio haki, asiye na hatia kwa wenye hatia, ili kwamba heshima ya sheria ya Mungu ihifadhiwe na mwanadamu asipotee kabisa....
Mungu hajamnyima mwanadamu kitu chochote ambacho kingemfanya awe mwenye furaha au kumpatia utajiri wa milele. Ameufunika ulimwengu kwa uzuri, na kuujaza kwa kila kitu ambacho ni lazima kwa ajili ya starehe ya mwanadamu katika maisha yake ya muda mfupi.
—The Signs of the Times, Juni 2, 1887.
154
Post a Comment