NDUMBARO AWASIHI WATUMISHI, CHEO NI DHAMANA
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amewataka Watumishi wa Umma waliopewa dhamana ya kuwasimamia na kuwaongoza watumishi walio chini yao kutambua
kwamba, cheo ni dhamana, hivyo wanapaswa kutumia vyeo vyao vizuri kuwahudumia wananchi na wanaowasimamia badala ya kujikweza.
Dkt. Ndumbaro ametoa wito huo kwa Watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Katavi, Manispaa ya Mpanda na Halmashauri za Wilaya ya Nsimbo na
Tanganyika wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Katavi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji pamoja na kusikiliza na kutatua kero na changamoto
zinazowakabili watumishi walio katika maeneo ya pembezoni mwa nchi.
Amesema hakuna haja ya wenye madaraka katika Utumishi wa Umma kuwakandamiza waliochini yao, bali wanapaswa kutengeneza mazingira ya
amani mahala pa kazi ili wao na wanaowasimamia washiriki kuujenga utumishi wa umma wenye msingi imara wa maadili na unaozingatia Kanuni, Sheria, Taratibu na Miongozo iliyopo.
"Mamlaka uliyonayo katika utumishi wa umma si lazima uyaonyeshe kwa mabavu na kujikweza kwani jamii inatambua na kukuheshimu kwa cheo au nafasi uliyonayo", Dkt. Ndumbaro amesisitiza.
Ameongeza kuwa, cheo ni kama koti tu kwani ipo siku utalivua na litavaliwa na mwingine aidha kwa kustaafu au Serikali kumpatia mwingine cheo
hicho, hivyo amewataka watumishi waliopo mkoani au makao makuu ya taasisi yoyote ile kutojiona kuwa ni bora kuliko wengine.
Amewakumbusha viongozi waliopo katika utumishi wa umma kuwahudumia wengine vizuri ili pindi watakapostaafu na kurejea kupata huduma katika ofisi walizokuwa wakiziongoza wapokelewe kwa heshima
na kuhudumiwa vizuri.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Katavi, Bw. Abdallah Malela amesisitiza utekelezaji maelekezo aliyoyatoa Dkt. Ndumbaro
kwa kuwataka Watumishi wa Umma mkoani Katavi kufanya kazi kwa uadilifu na uzalendo mkubwa na kuongeza kuwa, huo ndio utamaduni
unaopaswa kuzingatiwa na mtumishi yeyote wa umma.
Dkt. Ndumbaro amehitimisha ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Songwe, Rukwa na Katavi kwenye halmashauri zilizopo pembezoni, ziara ambayo
ililenga kuhimiza utendaji kazi wenye matokeo ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan anautaka katika utawala wake, Sanjali na hilo Dkt. Ndumbaro ametumia ziara hiyo kutatua changamoto na kero zinazowakabili Watumishi wa Umma waliopo maeneo ya pembezoni katika mikoa hiyo
Post a Comment