NA MALISA GJ PART 1

Mchakato wa kuifanya Chato kuwa mkoa umefikia hatua za mwisho kabisa. Kilichobaki ni mama Samia kuutangaza mkoa huo mpya kama atakubaliana na mapendekezo yaliyotolewa au kuyatupilia mbali mapendekezo hayo. May 26 ilikua siku ya kukamilisha taratibu za kisheria za kuifanya Chato kuwa mkoa.

Kamati ya ushauri cha Mkoa wa Geita, imeridhia kuanzishwa kwa mkoa mpya wa Chato na kupendekeza uwe na wilaya tano. Wilaya mbili zitamegwa kutoka mkoa wa Geita ambazo ni Chato na Bukombe. Mbili zitatoka mkoa wa Kagera ambazo ni Biharamulo na Ngara. Na moja itamegwa kutoka Kakonko mkoani Kigoma. Pia baadhi ya kata za wilaya Muleba zitahamishiwa Chato.

Mkoa wa Kagera una wilaya 7 ambazo ni Bukoba, Misenyi, Muleba, Karagwe, Ngara, Biharamulo na Kyerwa. Kwahivyo Biharamulo na Ngara zikipelekwa mkoa mpya wa Chato, Kagera itabaki na wilaya tano.

Lakini mkoa wa Geita una wilaya 5 ambapo mbili zikitolewa kwenda mkoa mpya wa Chato zitabaki tatu ambazo kisheria haziwezi kuunda mkoa. Kwahiyo imependekezwa mkoa wa Geita uongezewe wilaya mbili. Moja ni Sengerema kutoka Mwanza na nyingine ni Busanda ambayo itamegwa kutoka maeneo ya mkoa wa Shinyanga na Geita.

Kuanzishwa kwa mkoa wa Chato kumeathiri mikoa ya Kagera, Kigoma, Geita, Mwanza na Shinyanga. Zaidi ya mikoa mitano imeguswa ili tu kuwezesha mkoa wa Chato kupatikana. Hali hii imefanya baadhi ya watu kulalamika kuwa Chato IMELAZIMISHWA kuwa mkoa na haina vigezo.

Mmoja kati ya waliolaani Chato kuwa mkoa ni Prof.Anne Tibaijuka Mkurugenzi mstaafu wa shirika la makazi duniani (UN-Habitat) na Waziri mstaafu kwenye wizara mbalimbali. Prof.Tibaijuka ameandika maoni yafuatayo;

Chato haina sifa ya kuwa mkoa. Tusidanganyane. Ramani inaonyesha Chato ni sehemu ya Wilaya ya Biharamulo Mkoa wa Kagera. Kiuhalisia na kihistoria. Mengine ni kulazimishalazimisha tu. Naendelea kusisitiza hakuna hoja yoyote ya kiuchumi kuunda mkoa wa Chato. La sivyo basi tuelimishwe.

Ila kama mnapenda siasa za upendeleo wa sehemu fulani ama kwa kuwa mkubwa aliwahi kuzaliwa pale au mtu apewe nafasi kwa sababu ni mtoto wa kiongozi endeleeni kuwabebesha wananchi mizigo ya kulipa kodi kusudi wateule wajichane. Period.

No comments