RAIS DR. HUSSEIN ALI MWINYI: INAPENDEZA KUONA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA SASA INAUNGANA NA MATAIFA MENGINE DUNIANI KATIKA KUKUZA NA KUIMARISHA MASHINDANO YA KUSOMA NA KUHIFADHI QURAN


Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo katika hafla ya mashindano ya 21 ya Qurani ya juu 30, yaliyofanyika katika uwanja wa Benjamin William Mkapa Jijini Dar-es-Salaam na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali pamoja na maelfu ya wananchi.
 
Katika hotuba yake, Rais Dk. Mwinyi aliwataka Watanzania kuona kuwa ushiriki wao katika mashindano hayo ni fursa adhimu ya kuitangaza Tanzania kama inavyofanya katika mashindano mengine ya Kitaifa inayoshiriki.
 
Alisema kuwa ni jambo jema na la kheri kushuhudia kwamba mashindano ya Kuhifadhi Qurani, kitabu kitukufu cha Mwenyezi Mungu yanazidi kupata nguvu na umaarufu duniani hivi sasa.
 
Aliongeza kuwa nchi mbali mbali zinaendelea kuandaa mashindano hayo kwa ngazi ya Kitaifa na Kimataifa huku akitumia fursa hiyo kuipongeza Taasisi ya Al-Hikma kwa kuandaa mashindano hayo.
 
Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa Watanzania wa rika mbali mbali wamekuwa wakionesha umahiri mkubwa katika mashindano na kupeperusha bendera ya nchi yao Kimataifa, katika mataifa kadhaa ikiwemo Saud Arabia, Iran,Oman, Malaysia na nchi nyenginezo.
 
Hivyo, Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba ni vyema kwa madrasa za hapa nchini pamoja na taasisi nyengine za dini ya Kiislamu zikahakikisha kwamba zinawaandaa vizuri vijana wenye vipaji vya kuhifadhi Quarani ili pale wanaposhiriki waiwakilishe vyema Tanzania na warejee nyumbani wakiwa na zawadi na tunzo mbali mbali.

No comments