waziri biteko afafanua malalamiko ya wachimbaji wadogo mirerani
Mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro, Mkoani Manyara juzi, Mhandisi Zephania Chaula, wadau hao wa madini walidai huwa wanadhalilishwa kwa kuvuliwa nguo mbele ya watu huku wakiangaliana kama wanyama.
Hata hivyo, jana Mwananchi lilizungumza kwa simu na Waziri Biteko ambaye alisema si lengo la Serikali kutweza utu wa mtu, hivyo malalamiko yao yanafanyiwa kazi.
“Utu wa mtu lazima uheshimiwe, serikali haipo kwa ajili ya kutweza utu wa watu bali kuulinda na uheshimiwe,” alisema.
Lakini pia alisema ili kukabiliana na tatizo hilo, tayari Serikali imeanza hatua ya kujenga vyumba vinne vitakavyotumika kwa ukaguzi huku wakiandaa utaratibu wa upatikanaji wa mashine ya ukaguzi.
“Ila wachimbaji nao hebu wajiulize, kwa nini tunafikia hatua ya kuanza kukaguana kwa kiwango hiki? Kuna tabia imezuka hivi karibuni kwa baadhi ya wachimbaji kujaribu kutorosha madini kwa kuyaficha sehemu zisizodhaniwa,” alisema Biteko.
Alisema wapo waliokamatwa wakiwa wameyaficha madini hayo kwenye nguo za ndani na wengine wanayaficha sehemu za siri.
Alisema wizi huo ndiyo uliochangia ukaguzi wa kuvuana nguo uanze. “Sasa kama wanaona njia hii inawadhalilisha na wanataka wakaguliwe kistaarabu, waache basi wizi huu, watusaidie kuwataja wanaowaona wanafanya vitendo hivi,” alisema Waziri huyo.
Hata hivyo alisema wataendelea kuhimiza ukaguzi wa kistaarabu usio na chembe ya udhalilishaji.
Akizungumza juzi kwenye mkutano wa wadau hao, mmoja kati ya wachimbaji hao, Abubakary Madiwa alisema kosa la mtu mmoja kutorosha madini ya Tanzanite isiwe kigezo na chanzo cha kuwadhalilisha watu wengine kuvuliwa nguo.
Turusia Chande, alisema hayati Mwalimu Julius Nyerere alikemea utu wa mtu kudhalilishwa na Rais John Magufuli anafuata itikadi za Nyerere akisikia hayo yanafanyika kwa watu kuvuliwa nguo ili kupekuliwa atasikitika sana
Mdau mwingine mchungaji Ufoo alisema kitendo cha watu 10 kuvuliwa nguo na kubaki watupu mkiangaliana kiliwahi kutokea kipindi ha utumwa na sasa kwenye Tanzanite.
Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mhandisi Chaula alisema upekuaji huo umefanyika kutokana na utoroshaji wa madini unaofanyika kupitia maungoni mwa baadhi ya watu.
Alisema baadhi ya wanaume wamekuwa na tabia ya kuweka madini hayo kwenye makalio
“Kuna baadhi ya wanawake walikamatwa kwa kupitisha madini hayo kwa kuweka vitambaa vya rangi nyekundu kwenye sehemu zao za siri na kusababishia wanawake wengine matatizo,” alisema Chaula.
Post a Comment