juma mahadhi: Sitokuja kuisahau yanga

Winga wa Klabu ya Yanga aliyeko kwa Mkopo Ihefu FC,Juma Mahadhi amesema hatokuja kuisahau Klabu ya Yanga kwenye maisha yake ya mpira kwani kama isingekuwa msaada kutoka kwao, basi huenda angekuwa mlemavu wa mguu Mpaka sasa.

“Yanga ni timu yangu ambayo siwezi kuisahau katika maisha yangu, kwani mbali na kuwa mchezaji tu lakini uongozi uliniona kama mtoto wao na kunijali pale nilipopatwa na mapito.”

Anasema, kwa mazingira na magumu aliyoyapitia kupitia kutokana na majeraha hayo, imekuwa funzo kubwa kwake kutokata tamaa na kuamini Mungu yupo na kila jambo linakuja kwa wakati wake na sababu pia.

KUONDOKA YANGA

Baada ya kupona na kurejea katika majukumu yake kama zamani, iliwafanya Yanga kumtafutia timu ya Ihefu ili akacheze kwa mkopo kwa ajili ya kurejesha kiwango chake kama hapo zamani.

“Hata viongozi walivyoniita na kuniambia wananipeleka huko na sababu walizonieleza niliona ni sawa kabisa kutokana na kukaa kwangu muda mrefu na upinzani uliokuwepo kwa sasa mimi kutoka majeruhi na kupata nafasi najua ingekuwa ngumu.”

“Walivyoniita na kuniambia hata mimi niliona ni kweli wana hoja na wananitakia mema katika maisha yangu ya soka, napambana huku makazi mapya ninaamini ipo siku nitarejea tena Yanga,” anabainisha nyota huyo.

Anasema kwa faida yake akaridhia vilivyo kuondoka ili kulinda kiwango chake kuliko kukaa Yanga bila ya kupata nafasi ya kucheza.

MAZINGIRA YA SASA

“Nilipotoka na nilipo ni tofauti sana tu, ila mazingira nimeyazoea haraka wachezaji ni familia kama kwingine tu nilikotoka mkiwa pamoja mnaelewana haraka, najivunia na nafurahi kuwa sehemu ya wachezaji wa Ihefu.”

“Napambana kuhakikisha napata nafasi ya kwanza ndani ya kikosi, nia na uwezo ninavyo, nikipata mimi nafasi sawa akipata mwenzangu sawa, kwa kuwa wote ni timu na tunafanya kazi moja tu.”

HATOSAHAU HIKI KUMBE

Mahadhi anasema, katika maisha yake kitu ambacho hawezi kukisahau ni ni siku ambayo walicheza na USM Alger akiwa na Yanga mwaka 2019 na kuumia goti lililomweka nje ya dimba miaka miwili.

“Siwezi kusahau, kwani ni kipindi kigumu ambacho nilikipitia na sitokisahau katika maisha yangu, maana goti lilinikosesha mambo mengi sana, sikuweza kufanya kazi yangu ipasavyo na kubakia kuuguza majeraha ila namshukuru mungu.”

“Nilikuwa na wakati mbaya ambao ni zaidi ya maumivu yaliyoingia katika historia ya maisha yangu kusahau ni ngumu sana, namwomba Mungu isijetokea tena, maana goti lilinitesa sana mpaka niliwaza mbali huenda ningepata ulemavu,” anasimulia kwa uchungu na kuongeza, kilimuumiza kwani hakujua ni lini atarejea kama kawaida.

FURAHA ASIYOISAHAU

“Yaani nilijiona dunia nyingine, nilikuwa mtu mwenye furaha sana, kwa kuona uongozi wangu unanijali sana, licha ya kuumwa lakini nilipata kila kitu.”

“Zamani walisema mchezaji akiumia anaachwa, lakini niliona hayo maneno sio ya kweli, kwani kuna wachezaji waliondoka mimi nikabakia basi nilizidi kuwa na furaha ambayo haikuweza kusemeka kwangu.”

MALENGO YAKE

“Napambana natamani pia mashabiki zangu wajue na waamini mimi nimerejea na kupambana kurejea kama kama zamani nilivyokuwa, kwa jitihada zangu najua nitafikia tu.”

TIMU YA TAIFA

“Naamini kwa timu ya Taifa ni ya wote ni suala la muda tu, pia Mungu tu anapanga wakati ukifika angalia mashindano ya Chan walikuwa wachezaji wapya wengi ambao kila mtu hakutarajia hivyo itakuwa tu.

WACHEZAJI WAGENI

“Wageni wanatufanya sisi tuzidi kujituma zaidi na zaidi, mbona Miraji yuko Simba anapata namba, kina Metacha anacheza na Faruk yuko pale hata Kaseke mbona anaanza Sarpong anasubiri ni kujiamini tu na kuwa na malengo yako kama mchezaji.”

MBIONI KUVUTA JIKO

Ndoa ni jambo la kheri na ni moja ya ibada kwa kila mwanadamu endapo ametimiza umri kuanzia miaka 18, hivyo basi mara baada ya ligi kutamatika Mahadhi anatarajia kuvuta jiko.

“Nimekaa peke yangu imetosha sasa ni wakati wa kutafuta mwenzangu wa kuishi nae, kwa sasa niko bize na kazi kwanza ligi ikimalizika nitaoa.”

NENO KWA MASHABIKI

“Mashabiki wajitahidi sana kuwasapoti wachezaji wetu, usimjaji mtu kutokana na mwonekano wa nje, wafanye wachezaji wawe na furaha na wajue kila mtu ana kitu anakipenda na sio kila mtu kumfurahisha kwa kile unachokiamini.”

No comments