amka na Bwana leo 4
KESHA LA ASUBUHI
ALHAMISI, MACHI, 4, 2021
SOMO: KILA HATUA KATIKA NJIA
Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu.
Waefeso 2:8.
Hatuwezi hata kuitengeneza imani sisi wenyewe. “Ni kipawa cha Mungu; (Waefeso 2:8). Wokovu wetu wote huja kwa njia ya kipawa cha Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Nina furaha kiasi gani. Unakuja toka katika chanzo ambacho hatuwezi kukitilia mashaka, Naye ni “mwenye kuanzisha” —je, hukomea hapo? “Mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu” (Waebrania). Ashukuriwe Mungu. Hutuhudumia kila hatua katika njia, ikiwa tuko tayari kuokolewa kupitia njia iliyoteuliwa ya Kristo, kupitia utii wa matakwa yake. Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu; ni kipawa cha Mungu” (Waefeso 2:8).
“Utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka” (Wafilipi 2:12). Hii humaanisha nini? Je, ni mkanganyiko? Hebu tuone mwisho wake husema nini. "Utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka. Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.” (Fungu la 12,13).
Mungu Atukuzwe. Sasa ni nani atakayekatishwa tamaa? Ni nani atakayezimia? Hatukupatiwa sisi, tufao, wadhaifu, wanyonge kuutimiza wokovu wetu wenyewe kwa njia yetu wenyewe. Ni Kristo ndiye atendaye kazi ndani yenu. Na huu ni upendeleo wa kila mwana na binti wa Adamu. Lakini tunapaswa kufanya kazi. Hatupaswi kukaa bila kazi. Tumewekwa katika ulimwengu huu kufanya kazi. Hatukuwekwa hapa kukunja mikono yetu.
Kristo aliifundisha kweli kwa sababu yeye alikuwa Ndiye kweli. Wazo Lake mwenyewe, tabia Yake mwenyewe, uzoefu wa maisha yake, vilijumuishwa katika mafundisho yake. Hivyo pamoja na watumishi wake; wale ambao wangelifundisha neno wanapaswa kulifanya kuwa uzoefu wao binafsi. Ni lazima wajue kile kinachomaanishwa kuwa Kristo alifanywa kwao hekima na haki na utakaso na ukombozi. Katika kuliwasilisha Neno la Mungu kwa wengine, hawapaswi kuliweka kama ‘huenda ni hivyo,’ au 'labda' Wanapaswa kutamka pamoja na mtume Petro, “Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake” (2 Petro 1:16)....
Kadiri mtenda kazi anavyojitoa kikamilifu kwa ajili ya utumishi wa Bwana, anapata uzoefu unaomwezesha kufanya kazi zaidi na zaidi kwa mafanikio kwa ajili ya Bwana.
Post a Comment