amka na Bwana leo 26
KESHA LA ASUBUHI
IJUMAA, MACHI, 26, 2021
SOMO: KUJITENGA NA DHAMBI
Basi ikiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi.
Wakolosai 3:1, 2.
Maagizo ya Mungu yamewekwa kwa uwazi mbele yetu, na swali linalopaswa kujibiwa ni, Je, tutayatii? Je, tutayakubali masharti yaliyowekwa katika Neno lake —kujitenga na dunia? Hii si kazi ya muda kidogo au siku moja. Haikamilishwi kwa kupiga magoti katika madhabau ya familia, na kutoa huduma ya maneno matupu, wala si kwa ushawishi wa hadhara na maombi. Ni kazi ya maisha yote.
Kujiweka kwetu wakfu kwa Mungu ni lazima iwe kanuni hai, iliyofungamana na maisha, na kutuongoza katika kujikana nafsi na kujitoa kafara. Ni lazima iwe msingi wa mawazo na kuwa chemchemi ya kila tendo. Hii itatuinua juu ya ulimwengu, na kututenga na mvuto wake unaochafua. Matendo yetu yote yanaathiriwa na uzoefu wetu wa kidini, na ikiwa uzoefu huu umejengwa juu ya Mungu na tunaelewa siri za utauwa, ikiwa kila siku tunapokea toka katika nguvu ya ulimwengu ujao, na kuwa na ushirika na Mungu, na kuwa na ushirika na Roho Mtakatifu, ikiwa kila siku tunadumu kushikilia kwa uimara maisha ya juu, na kusogea karibu tena karibu zaidi na bubujiko la Mwokozi, tutajipamba ndani yetu kanuni ambazo ni takatifu na za milele.
Kisha itakuwa kama kawaida kwetu kutafuta usafi na utakatifu na kujitenga kutoka katika dunia, kama ilivyo kwa malaika wa utukufu kutekeleza utume wa upendo waliopewa katika kuokoa wanadamu wafao kutoka katika mvuto unaoharibu wa dunia. Kila mmoja anayeingia katika malango ya lulu katika mji wa Mungu atakuwa mtendaji wa Neno. Atakuwa mshirika wa tabia ya uungu, kwa kuokoka toka katika upotovu uliopo duniani kupitia kwa tamaa.
Ni fursa yetu kutambua utimilifu unaopatikana ndani ya Kristo, na kubarikiwa kwa upaji kupitia kwake. Utoaji mkubwa umefanyika kwamba tuinuliwe toka katika nyanda za chini za dunia, na kuwa na mapenzi yetu yakiwa yamekazwa kwa Mungu na mambo ya mbinguni. Je, huku kujitenga toka duniani katika utii kwa agizo takatifu, hakutatufaa kwa ajili ya kufanya kazi ambayo Bwana ametuachia? Hapana; kadiri tunavyoshikilia mbingu kwa uimara, ndivyo nguvu yetu itakuwa na manufaa makubwa katika ulimwengu.
Post a Comment