mafunzo ya watu wazima leo 2
LESONI, FEBRUARI 2
SOMO: ANGUKO LA “MFALME” WA MLIMA (ISAYA 14)
Kama matokeo ya anguko la Babeli (Isaya 13), jambo ambalo linawaweka huru watu wa Mungu (Isa. 14:1—3) Isaya 14:4—23 inatumia maneno ya dhihaka kwa lugha ya picha (tazama pia Mik. 2:4, Hab. 2:6) dhidi ya mfalme wa Babeli. Ni lugha ya kishairi ambayo haikukusudiwa ieleweke moja kwa moja, kwa hakika, kwani inaonesha wafalme waliokufa wakimsalimia mwenzao katika ulimwengu wa wafu (Isa. 14:9, 10), ambapo funza na wadudu ni kitanda chake (Isa. 14:11). Hii ni lugha ya picha ambayo Bwana anaitumia kumwambia mfalme mwenye kiburi kuwa atashushwa chini, kama wafalme wengine waliokuwapo kabla yake —siyo ufafanuzi kuhusu hali ya wafu!
Isaya 14:12—14 inawezaje kutumika kumaanisha mfalme wa Babeli?
Wafalme wa Babeli hawakuwa na tatizo la kutojithamini (Danieli 4, 5). Lakini kutamani kufanana "na yeye Aliye juu" (Isa. 14:14) lingekuwa jambo la ubinafsi uliokithiri. Wakati wafalme walidai kuwa na mahusiano ya karibu sana na miungu, walikuwa bado chini ya miungu. Jambo hili lilithibitika kila mwaka siku ya tano ya Siku Kuu ya Mwaka Mpya wa Babeli, ambapo mfalme alipaswa kuondoa alama yake ya kifalme kabla ya kuikaribia sanamu ya Marduk ili ufalme wake uthibitishwe upya. Wazo la kuchukua nafasi ya mungu hata aliye mdogo kabisa lingetazamwa kama la kipumbavu na la kujinyonga.
Kama ilivyo katika Isaya 14, Ezekieli 28 inahusisha kiburi kinachogusa mambo ya mbinguni na mfalme wa mji. Hapa pia, maelezo yanapita ya mfalme wa duniani, na kiumbe aliye karibu na Mungu anahusishwa: Mfalme mwenye kiburi alikuwa katika Bustani ya Edeni, kerubi aliyepakwa mafuta, afunikaye, au mlinzi kwenye mlima mtakatifu wa Mungu, mkamilifu tangu siku alipoumbwa mpaka dhambi ilipoonekana ndani yake, ambaye Mungu alimtupa nje, na ambaye hatimaye ataangamizwa kwa moto (Eze. 28:12—18).
Maelezo haya yakitumiwa kwa mwanadamu ye yote, maneno mahsusi, yaliyotumika ni ya picha za hali ya juu mno kiasi kwamba yangekosa maana. Lakini Ufunuo 12:7—9 inaelezea kiumbe mwenye nguvu sana aliyetupwa chini kutoka mbinguni akiwa na malaika zake: “Shetani, audanganyaye ulimwengu wote” (Ufu. 12:9), aliyemdanganya Hawa katika Bustani ya Edeni (Mwanzo 3).
Shetani fikra zilizojaa kiburi: " .... nawe umesema, Mimi ni Mungu, nami nimeketi katika kiti cha Mungu, kati ya bahari,’ lakini u mwanadamu wala si Mungu" (Eze. 28:2). Kifo chake kitathibitisha kuwa yeye siyo Mungu. Tofauti na Kristo, Shetani ataangamizwa katikati ya bahari ya moto (Ufu. 20:10), asiweze kusumbua ulimwengu tena.
Linganisha Isaya 14:13, 14 na Mathayo 11:29, Yohana 13:5, na Wafilipi 2:5—8. Tofauti hii inatuambia nini kuhusu tofauti kati ya tabia ya Mungu na tabia ya Shetani? Tofauti hii inatuambia nini kuhusu mtazamo wa Mungu juu ya kiburi, kujiinua, na shauku ya ukubwa?
Post a Comment