mafunzo ya watu wazima leo 31

LESONI, JANUARI 31

SOMO: HUKUMU DHIDI YA MATAIFA (ISAYA 13)



Isaya 13:1 inamtaja Isaya kuwa ndiye mwandishi (linganisha na Isa. 1:1, Isa. 2:1); inaonekana, pia, inaanza sehemu mpya ya kitabu chake. Sura 13—23 zina matamko ya hukumu dhidi ya mataifa mbalimbali. Hebu tuangalie. 



Kwa nini matamko ya kiunabii dhidi ya mataifa huanza na Babeli?

Isaya 10:5—34 ilikuwa tayari imeshatangaza hukumu dhidi ya Ashuru, ambayo ilikuwa hatarishi zaidi kuliko mataifa yote wakati wa Isaya. Wakati Isaya 14:24—27 hueleza kwa kifupi mpango wa Bwana wa kuivunja—vunja Ashuru, sura za 13—23 hushughulikia mataifa makubwa hatarishi mengine, Babeli ikiwa ndiyo muhimu kuliko mengine yote. 



Likiwa limejaliwa urithi mkubwa wa zamani wa kiutamaduni, kidini, na kisiasa, Babeli baadaye iliibuka kuwa taifa lenye nguvu sana ambalo lilishinda na kuwachukua mateka watu wa Yuda. Lakini kwa mtazamo wa kibinadamu wa wakati wa Isaya, isingekuwa rahisi kuamini kuwa Babeli ingekuwa tishio kwa watu wa Mungu. Katika kipindi kirefu cha huduma ya Isaya, Ashuru iliitawala Babeli. 



Tangu 728 K.K., Tiglath-pileseri III alipoiteka Babeli na kutangazwa kuwa mfalme wa Babeli kwa kiti cha enzi kilichoitwa Pulu (au Pul; tazama 2 Wafalme 15:19, 1 Nya. 5:26), wafalme wa Ashuru waliiteka Babeli mara kadhaa (710 K.K., 702 K.K., 689 K.K., and 648 K.K.). Babeli, hata hivyo, hatimaye ilikuja kuwa taifa lenye nguvu nyingi katika ukanda ule, mamlaka ambayo baadaye iliuangamiza ufalme wa Yuda. 



Soma Isaya 13 yote. Angalia jinsi lugha ilivyo na nguvu. Kwa nini Mungu mwenye upendo anafanya mambo haya, au anaruhusu mambo haya yatokee? Hakika baadhi ya watu wasiokuwa na hatia wangeteseka, pia, wasingeteseka (Isa. 13:16)? Tendo hili la Mungu tunalielewaje? 



Aya hizi, na aya zingine katika Biblia zinazozungumzia hasira na chuki ya Mungu dhidi ya dhambi na uovu zinatuambia nini kuhusu dhambi na uovu? Je, siyo kwa sababu Mungu mwenye upendo anatenda hivyo kutupatia ushahidi wa jinsi dhambi ilivyo mbaya? Inatupasa tukumbuke kuwa huyu ni Yesu anayesema kupitia kwa Isaya, Yesu yule yule aliyesamehe, aliyeponya, aliyewasihi na kuwakemea wenye dhambi ili watubu. 



Kwa akili zako binafsi, unaelewaje suala hili la tabia ya Mungu mwenye upendo? Jiulize swali hili, pia: Hasira hii haiwezi kuwa inatokana hasa na upendo Wake? Ikiwa ni hivyo, ni kwa jinsi gani? Au, hebu liangalie kwa mtazamo mwingine, ule wa Msalaba, ambapo Yesu Mwenyewe, akibeba dhambi za ulimwengu, aliteseka zaidi kuliko mwanadamu mwingine ye yote aliyewahi kuteseka, hata wale “watu wasio na hatia” walioteseka kwa sababu ya dhambi za taifa. 




Mateso ya Kristo Msalabani yanakusaidiaje kujibu haya maswali magumu? 

No comments