mafunzo ya watu wazima leo 28
LESONI, JANUARI 28
SOMO: “ULINIFARIJI” (ISA. 12:1—6)
Isaya 12 ni zaburi (wimbo) fupi ya kumsifu Mungu kwa ajili ya faraja Yake ya rehema na yenye nguvu. Zaburi, ikiwekwa katika mdomo wa mmojawapo wa waliosalia waliorudishwa, hulinganisha ukombozi ulioahidiwa na kukombolewa kwa Waebrania kutoka Misri (tazama Isa. 11:16); ni kama wimbo wa Musa na Waisraeli wakati walipookolewa dhidi ya jeshi la Farao kwenye Bahari ya Shamu (tazama Kutoka 15).
Linganisha wimbo huu katika Isaya 12 na Ufunuo 15:2—4, wimbo wa Musa na wa Mwanakondoo. Wanamsifia Mungu kwa jambo gani?
Isaya 12:2 hukaribia kabisa kutambulisha Mkombozi anayekuja kuwa ni Yesu. Aya inasema kuwa “Mungu ni wokovu wangu” na
“amekuwa wokovu wangu.” Jina Yesu humaanisha "Bwana ni Wokovu" (linganisha Mathayo 1:21).
Nini umuhimu wa wazo, lililomo katika jina la Yesu, kuwa Bwana ni wokovu?
Siyo tu kuwa Bwana anatenda wokovu (Isa. 12:2); Yeye Mwenyewe ni wokovu. Uwepo wa Mtakatifu wa Israeli katikati yetu (Isa. 12:6) ni vyote kwa ajili yetu. Mungu yupo pamoja nasi! Siyo tu kuwa Yesu alitenda miujiza; “alifanyika mwili na aliishi miongoni mwetu” (Yohana 1:14, mkazo umeongezwa). Siyo tu kuwa alibeba dhambi zetu msalabani; alifanyika dhambi kwa ajili yetu (2 Kor. 5:21). Siyo tu kuwa analeta amani; Yeye ni amani yetu (Efe. 2:14).
Siyo ajabu “shina la Yese lisimamalo kuwa ishara kwa kabila za watu, yeye ndiye ambaye mataifa watamtafuta” (Isa. 11:10). Alipoinuliwa juu ya msalaba, aliwavuta wote Kwake (Yohana 12:32, 33)! Waliosalia watarudi kwa "Mungu mwenyezi" (Isa. 10:21), ambaye ni Mtoto aliyezaliwa kwa ajili yetu, “Mfalme wa Amani” (Isa. 9:6)!
Tafakari kwa kina juu ya wazo hili kuwa Yesu ni wokovu wetu. Soma Warumi 3:24. Aya inasema kuwa ukombozi upo katika Yesu; ukombozi ni kitu kilichotokea ndani Yake, na ni kwa njia ya neema na rehema za Mungu kuwa tunaweza kuwa na sehemu ya milele katika ukombozi huo, pia. Kwa maneno mengine, ukombozi huo ambao ulikuwa ndani Yake unaweza kuwa wetu kwa imani, na siyo kwa matendo yetu, kwa kuwa hakuna matendo tunayoyafanya ni mema kiasi cha kuweza kutukomboa. Matendo ambayo Kristo pekee aliyafanya, ambayo anatuhesabia kwa imani, yanaweza kuleta ukombozi.
Ukweli huu unakupaje tumaini na hakika ya wokovu, hususani unapozidiwa na hisia za kutokufaa kwako?
Post a Comment