Furaha Dominic aliyeshinda kura za maoni Kawe ametoa maoni yake kwa Gwajima kupitishwa na Magufuli
Furaha Dominic, aliyeongoza katika kura za maoni kati ya walioomba nafasi ya kugombea ubunge katika jimbo la Kawe jijini Dar es Salaam kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), amezungumza saa chache baada ya chama hicho kumpitisha Askofu Josephat Gwajima aliyeshika nafasi ya tatu katika kura hizo.
Dominic amewaambia waandishi wa habari kuwa uamuzi uliofanywa na chama hicho ni sahihi, na kwamba kinachofuata sasa ni kumuunga mkono Askofu Gwajima ili aweze kumshinda mpinzani wake katika jimbo hilo, Halima Mdee aliyepitishwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwania tena ubunge wa jimbo hilo.
“Natoa shukurani zangu kwa wajumbe na nasema nimekubaliana na maamuzi ya chama na nitamuunga mkono huyo aliyependekezwa na chama, Ndugu Askofu Gwajima, lengo letu ni moja tu kama vijana wana CCM ni kukirudisha chama madarakani,” amesema.
“Tunaamini chama kimemchagua mtu sahihi na tunaamini sisi ni asset ya kesho kwa ajili ya chama chetu, na nataka niwaambie wajumbe wote walichukulie hili jambo kwa furaha. Ni jambo ambalo limefanyika kwa umakini na wamefanya kwa kufuata vigezo vingi, na naamini chama hakijakosea,” ameongeza.
Julai 21, 2020, wajumbe wa CCM katika jimbo hilo walimpigia Dominic kura 101 kati ya 474, Angela Kiziga alipata kura 85 akishika nafasi ya pili na Askofu Gwajima alipata kura 79.
Post a Comment