Askofu Kakobe Aionya Njombe

Dar es Salaam . Askofu mkuu wa kanisa la Full Gospel Bible fellowship (FGBF) Zakary Kakobe amewaonya watu wote wanajihusisha na matukio ya mauaji ya watoto Mkoa wa Njombe kwa lengo la kupata utajiri ama nyadhifa za uongozi kuacha na kutubu kwani hakuna utajiri unaopatikana kwa njia za kuua mtu.

Kakobe amesema hayo leo, Jumapili Aprili 21 (2019 ) wakati ikihubiri katika ibada maalumu ya Pasaka ambapo amesema yaliyotokea mkoa wa Njombe ni ya aibu na chukizo mbele za Mungu na kwamba kuua mtu ndipo upate utajiri ni uongo wa mchana kweupe na kudai wanaofanya hivyo wanalenga kuleta maasi ndani ya taifa.

“Hakuna utajiri wa namna hiyo ,utajiri unakuja kwa kufanya kazi …hao waganga wanaowadanganya wao wenyewe ni maskini wanakaa mazingira ya kimaskini halafu wanakupa dawa ya kupata utajiri..naomba wote wanaojua wamefanya hivyo warudi magotini pa Mungu Watubu,” amesema .

Amesema wanachokifanya ni laana kwa nchi na taifa lao na kuaibisha Taifa na kwamba kuua watoto ili upate utajiri ni ujinga wa hali ya juu na kuwataka Watanzania wabadilike na kuondoa Imani hiyo kwani kifo cha Yesu kristo msalabani kilifunika nguvu za kiza na kuleta nuru.

“Huwezi kufanikiwa kwa ,kuamini nguvu za giza, pasaka hii amka na tambua nuru inang’aa gizani na wala giza haling’ari kwenye nuru na kwamba mwanadamu yeyote anayemwamini Kristo nguvu za giza hazimo ndani yake “amesema.

No comments