"Uraia wa Askofu Kakobe"Wazee mashuhuri wa kijijini kwake wathibitisha uraia wake



Askofu Kakobe
Swala la uraia wake ,utafiti wafika hadi kijijini kwake kwa wazazi wake

Baada ya kupiga kambi hapa wilayani Kakonko, kwa wiki mbili sasa, uchunguzi wangu umebaini pasipo shaka, kwamba, Idara ya Uhamiaji, Dar-Es-Salaam; imewatuma maafisa wapelelezi wawili, mwishoni mwa mwezi uliopita, wilayani hapa, ili kuchunguza uraia wa Askofu Mkuu Zachary Kakobe. Wapelelezi hawa wamefanya mahojiano na watu mbalimbali katika mji wa Kakonko, na vijiji vya Mbizi na Kanyonza; ambako ndiko nyumbani kwa Askofu huyo. Taarifa za uhakika zimethibitisha kwamba, wazee wote mashuhuri waliohojiwa katika vijiji hivyo, wamethibitisha kwamba Kakobe ni Mtanzania halisi, kwa kuzaliwa.

Maafisa hawa wa upelelezi, walikuja hapa Kakonko kufanya uchunguzi, ili kubaini kama Askofu Kakobe ni Mtanzania, au ni raia wa Burundi. Uchunguzi huu umefanyika baada ya Askofu huyo Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), kuhojiwa katika ofisi za Uhamiaji, Mkoa wa Dar-Es-Salaam, tarehe 9.4.2018.

Wapelelezi hawa, walifika hapa Kakonko, Jumatatu 30.4.2018, saa saba mchana, na siku hiyohiyo, walikwenda kijiji cha Mbizi, ambako ndipo yalipo makazi ya wazazi wa Askofu huyo, na kuwahoji wazee mashuhuri kijijini hapo. Miongoni mwa wazee waliohojiwa, siku hiyo, ni Mzee Ally Halimenshi Bidebhe, ambaye makazi yake yako mkono wa kushoto wa ghala la tumbaku, kwenye kona ukitokea kwenye nyumba ya Marehemu Frank Chiza Kakobe, ambaye ndiye baba yake Askofu Kakobe.

Wakati anahojiwa, Mzee Ally Bidebhe, alikuwa ni mzee sana na alikuwa anatolewa nje asubuhi kuota jua, kisha anarudishwa ndani jioni, ingawa alikuwa ni mzungumzaji mzuri mwenye kumbukumbu nzuri, na akili timamu. Mzee huyu amefariki siku chache zilizopita , baada ya mimi kupata wasaa wa kuzungumza naye; na amefariki kwa kifo cha asili, kutokana na umri mkubwa, na nilihudhuria katika mazishi yake. Nilipomhoji mzee huyo kabla ya kufa kwake, alisema kwamba wapelelezi hao walimwuliza asili ya Kakobe, ni Tanzania, au ni Burundi? Aliwashangaa na kuwauliza kama wao ni wageni Kakonko. Kisha akawaambia kwamba Mzee Frank Kakobe alikuwepo kijijini hapo zamani sana kabla kijiji hicho hakijaitwa kijiji cha Mbizi, wakati wa Operesheni Vijiji vya Ujamaa, mwanzoni mwa miaka ya sabini. Zamani hizo, kijiji hicho kilikuwa kinaitwa Kanyaga.

Akasema, Marehemu Frank Chiza Kakobe ni Mtanzania, Muha wa asili kabisa, na hakutokea Burundi. Wazazi na ndugu zake wengi, makazi yao ni kijiji cha Nyamalebe, ambacho baadaye kilibadilishwa jina na kuitwa kijiji cha Kanyonza, wakati wa Operesheni ya Vijiji vya Ujamaa. Yeye aliamua kujenga hapo ili kuwa karibu na mji wa Kakonko, kutokana na shughuli zake za Ualimu maana alikuwa ni Mwalimu.

Mwingine aliyehojiwa kijijini hapo, ni Mwenyekiti wa kijiji cha Mbizi, Mzee Maringo Petro Kasogote (0759517815), yeye vilevile, alieleza kwa msisitizo kwamba Marehemu Frank Kakobe na familia yake ni Watanzania halisi, na ni wakazi wa zamani sana katika kijiji hicho, na kwamba anavyojua yeye, hawana asili yoyote ya Burundi, bali ni Waha wa asili kabisa katika eneo hilo.

Siku hiyohiyo, saa 3 usiku, wapelelezi hao, walikwenda nyumbani kwa kaka yake Askofu Kakobe, anayeitwa Fredrick Frank Chiza Kakobe (0764113984), anayeishi kitongoji cha Kukimanga, pembezoni kidogo mwa mji wa Kakonko; na kumwambia anatakiwa kwenda ofisi ya Uhamiaji kesho yake 1.5.2018 ili kuhojiwa. Ingawa siku hiyo ilikuwa ni sikukuu, alikwenda ofisi ya Uhamiaji na mahojiano hayo yalifanyika.

Nilipata nafasi ya kuzungumza ana kwa ana na Fredrick Chiza Kakobe mwenye umri wa miaka 65, ambaye ni Mwalimu mstaafu na alinieleza historia ya maisha yake kwa kusema, "Askofu Mkuu Zachary Kakobe, ni mdogo wangu anayenifuata. Baba yetu ni mmoja Frank Chiza Kakobe, na mama yetu ni mmoja, Debora Paulo. Baba yetu alizaliwa mwaka 1927 na baada ya kusoma enzi za ukoloni katika shule za awali, na Chuo cha Walimu, Katoke Teachers Training College, mkoani Kagera, alikuwa Mwalimu katika shule mbalimbali nchini Tanzania, katika mikoa ya Tanga, Rukwa, Tabora, Shinyanga na Kigoma; na hatimaye alistaafu mwaka 1984, na kufariki mwaka 2009. Mama yetu alifariki mwaka 2013. Wote wamezikwa kijijini kwetu Mbizi, pembezoni mwa nyumba yao."

"Katika familia yetu, tulizaliwa watoto saba, mmoja tu ndiye aliyefariki, na sita bado tuko hai. Watoto wa kwanza walikuwa mapacha, waliozaliwa mwaka 1952, Joyce Frank Kakobe ambaye kwa sasa ni mjane, na yuko Mwanza kwa watoto wake na wajukuu zake, na pacha wake Janeth Frank Kakobe ambaye alifariki mwaka 1995. Kisha nikafuata mimi niliyezaliwa 26.4.1953; kisha wakafuatia Zachary Frank Kakobe (6.6.1955); Stephen Frank Kakobe (17.9.1957), ambaye yuko kijijini Mbizi; Christopher Frank Kakobe (17.10.1961), ambaye yuko Arusha; na mtoto wa mwisho katika familia yetu ni Magreth Frank Kakobe (0763561648), ambaye alizaliwa 29.12.1966, na anaishi kitongoji cha Kanyaga, pembezoni mwa mji huuhuu wa Kakonko; ingawa kwa sasa yuko safarini Mwanza".

Baada ya kusoma shule za awali, nilisoma shule ya sekondari ya Ufundi Ifunda, Iringa (1971-1974), kisha Chuo cha Ualimu Kleruu, Iringa (1976-1977), kisha nikaenda JKT Mafinga, Iringa (1977-1978). Baada ya hapo nikawa Mwalimu wa shule za msingi mbalimbali, katika wilaya ya Kibondo kama ifuatavyo: Shule ya msingi Kasanda (1978-1986), Shule ya msingi Kibuye (1986-1990), Shule ya msingi Maendeleo (1990-1992), Shule ya msingi Kigaga (1993-1997), na Shule ya msingi Itumbiko (1997-2013). Nilistaafu tarehe 25.4.2013."

Fredrick alieleza kwamba alipokwenda ofisi ya Uhamiaji, katika mahojiano, alitoa maelezo ya historia yake hiyo, na kujibu maswali mengine katika kuwathibitishia kwamba familia yao ni Watanzania halisi. Kisha baada ya mahojiano, aliongozana na maafisa hao wa Uhamiaji mpaka kwenye nyumba ya Marehemu Frank Chiza Kakobe, katika kijiji cha Mbizi, ambacho kiko kilomita mbili tu kutoka Kakonko mjini, na wakapiga picha ya nyumba hiyo, na makaburi ya baba na mama yao, na pia wakapiga picha pamoja na Fredrick akiwa na mdogo wake Stephen Frank Kakobe. Maafisa hao walisema kwamba walizitaka picha hizo, kwa ajili ya kumbukumbu zao.

Siku iliyofuata, wapelelezi hao wa Idara ya Uhamiaji waliambatana na Mwenyekiti wa kijiji cha Mbizi, Maringo Petro Kasogote, na wakaenda kijiji cha Kanyonza, umbali wa kilomita tano hivi kutoka kijiji cha Mbizi, Hapa Kanyonza, ndipo penye asili na chimbuko la ukoo wa Kakobe. Ukoo wa Kakobe katika kijiji hiki, ni ukoo mkubwa sana na ndugu wengi wa ukoo huo wako eneo moja, na nyumba zao ziko eneo moja, ni kama kijiji fulani cha ukoo huo, ndani ya kijiji kikubwa cha Kanyonza.

Hapa Kanyonza, wapelelezi hawa, kwanza walifika kwa Marehemu Magambo Kakobe ambaye ni kaka yake Frank Chiza Kakobe, yaani baba yake mkubwa wa Askofu Kakobe. Hapa walikutana na mtu mwenye umri wa kama miaka 40 hivi, anayeitwa Kakobe Magambo Kakobe. Wakamwuliza, "Askofu Kakobe ni ndugu yako", akajibu "Ndiyo ni kaka yangu, marehemu baba yake ni mdogo wa baba yangu, marehemu Magambo Kakobe. Mimi nilipewa jina la Kakobe, kama jina la Babu yangu." Ukimwacha huyu Kakobe Magambo Kakobe, wako watoto wengi wa Magambo Kakobe hapa, kama Sylvester Magambo Kakobe, Ndaiwundi Magambo Kakobe, Nyakasase Magambo Kakobe na wengineo wengi, maana yeye alioa wake wengi. Vilevile, hapa kuna nyumba za ndugu zake Magambo Kakobe, kama Mzee Lazaro Bitwayiki (0758513660) mwenye umri wa miaka 67, ambaye wapelelezi hawa hawakumkuta, alikuwa shamba; na vilevile ziko nyumba za ndugu zake wengine ambao ni marehemu, kama marehemu Mzee Kitazi na wengineo.

Baadaye, maafisa hawa wa Uhamiaji walikwenda ofisi ya kijiji, na kukutana na Katibu Mtendaji Kata ya Kanyonza, akiwa pamoja na Katibu Mtendaji wa Kijiji cha Kanyonza; na kuwaambia wawaite hapo ofisini, wazee wa zamani walio mashuhuri, ambao walikuwepo wakati kijiji kinaanza, na wanaojua historia ya koo mbalimbali zilizoko katika kijiji.

Wazee mashuhuri walioitwa na kufika ofisini hapo, walikuwa ni Mzee Samweli Mibara, ambaye ni Mzee Mshauri na Mwenyekiti wa Wazee wa Kata ya Kanyonza; Mzee Kanaku Gwamuhizi (85) aliyetawala eneo hilo mwaka 1961 na 1962, akiwa ni msaidizi wa Mwami (Mtemi/Chief) Ruhaga, Mwami wa Muhambwe; na baadaye akawa Mwenyekiti wa Kijiji cha Kanyonza, kwa miaka kumi (1999-2009); na Mzee mwingine maarufu, Mzee John Chondi. Wazee hawa wote walitakiwa kueleza kila mmoja anaufahamu vipi ukoo wa Kakobe na kueleza pia kama hawa ni watu wa Burundi au ni Watanzania.

Kila mmoja katika wazee hawa alitoa maelezo yanayofanana kwa kiasi kikubwa na mwenzake, lakini kwa kifupi wote walisisitiza kwamba ukoo wa Kakobe ni Watanzania halisi na ni Waha wa Ukoo wa "Abhayango Abhazilankende", hivyo Askofu Kakobe ni Myango Mzilankende. Walieleza kwamba, ukoo wa Kakobe, ni moja kati ya koo za asili, katika kijiji cha asili cha Nyamalebe kilichokuwepo katika eneo hilo, kabla ya Operesheni ya Vijiji vya Ujamaa, mwaka 1974; iliyozaa Kijiji cha Kanyonza. Walisema kwamba, wakazi wa Nyamalebe wao hawakuhama, bali wakazi wa vijiji vingine vingi vya karibu na mbali, kama Bugunga, kilichokuwako baada ya mto Muhwazi, na vijiji vingine vya milimani, ndiyo waliohamishwa na kuletwa hapo. Hivyo ukoo wa Kakobe haukuhama, na hivyo babu zao wamefia hapo, na makaburi ya babu zao wa zamani bado yapo hapohapo. Walieleza kwamba, baba yake Askofu Kakobe, ni Frank Chiza, na Babu yake ni Kakobe, na baba yake Kakobe, yaani baba wa babu yake Askofu Zachary Kakobe, alikuwa anaitwa Ruzirumwolo, na wote wamefia hapo Nyamalebe, na makaburi yao wote, yapo hapo hata sasa.

Waliendelea kueleza kwamba, Mzee Frank Chiza Kakobe alizaliwa hapo Nyamalebe, na alikuwa anatokea hapo kwenda kusoma Kiziguzigu, baadaye Kibondo, na baadaye Chuo cha Ualimu Katoke, na kisha akawa Mwalimu, sehemu nyingi mbalimbali nchini.

Hatimaye Afisa mmojawapo wa Uhamiaji alimwuliza swali Mzee Kanaku Gwamuhizi, "Je, Kakobe ni jina la Kiha au ni la Kirundi? kama ni jina la Kiha, maana yake ni nini, na huwa linatolewa kwa mtu, katika mazingira gani ya kimila?" Mzee Kanaku alijibu, "Jina Kakobe, ni jina la Kiha halisi kabisa, siyo jina la Kirundi", kisha akaanza kueleza hatua kwa hatua, " Nyani (mnyama) katika lugha ya Kiha, tunamwita Nkobe (Nkobhe). Nyakati za mababu, enzi za ukoloni, mahali pengi kulikuwa hakuna leba hospitali au kliniki, hivyo wanawake wajawazito walikuwa hawaendi kujifungua leba hospitali, au kwenda kliniki, bali walikuwa wakijifungua mahali popote tu, kwa mfano nyumbani, shambani, chini ya mti, na kadhalika; kwa kusaidiwa na wakunga wa jadi, ambao waliwawezesha kujifungua salama. Sasa basi, huku Buha au kwetu Waha, tuna mti unaoitwa Mkobe (Umukobhe), ambao ni mti unaopendwa na nyani. Kama mwanamke mjamzito alishikwa na uchungu, na kisha akajifungua mtoto, akiwa chini ya mti wa Mkobe (Umukhobe); kama mtoto huyo akiwa ni wa kiume, aliitwa KAKOBE (Kakobhe); na kama mtoto huyo akiwa ni wa kike, aliitwa MKENKOBE (Mkenkobhe)".

"Vilevile, ikiwa mwanamke mjamzito alikuwa shambani akilinda nyani, ili wasile mazao; halafu akafika nyumbani au popote, hata iwe hospitali, halafu akajifungua mtoto, kama mtoto yule akiwa wa kiume aliitwa pia KAKOBE, na ikiwa ni wa kike aliitwa pia MKENKOBE, yaani alikuwa amekwenda kulinda nyani (Kiha tunasema: "Yali yagiye kulindi nkobhe"), kisha akarudi na kuzaa mtoto huyo."

Baada ya maelezo haya, Mzee Kanaku Gwamuhizi, aliwauliza maafisa hao, "Niwatajie wazee wengine maarufu hapa kijijini, ili waitwe waje nao kutoa maelezo?" Wakajibu, "Basi imetosha, tumetosheka, wala hatuendi mahali pengine, tumemaliza. Hatuna haja tena ya kuzungumza na mtu mwingine. Tunakwenda. Wewe ndiyo umefunga mlango. Hatuna haja ya maelezo mengine kutoka kwa yeyote mwingine. Inatosha." Baada ya maneno haya, maafisa hao wakaomba kupiga picha pamoja na wazee hao, na baada ya kupiga picha hizo, wazee hao wakaruhusiwa kuondoka.

Baadaye, Samweli Kibogo (0752338527), mwenye umri wa miaka 72, ambaye ni Mchungaji wa Kanisa la Anglikana Kakonko, na vilevile ni baba yake mdogo Askofu Kakobe; alipata taarfa kwamba jina lake lilitajwa na Fredrick Kakobe kule Uhamiaji, na wakapewa namba yake ya simu. Yeye naye akatamani sana kuhojiwa, lakini hakupigiwa simu wala kuitwa. Alivyosubiri kwa siku chache, alishindwa kuvumilia, akapata namba ya simu ya wale maafisa, na akawapigia simu na kuomba waonane. Wakamwambia wamekwisha kuondoka, wako Kigoma kwa shughuli nyingine, na hawana hakika kama watapata muda wa kuonana. Mpaka leo, hawajampigia simu, wala hawakurudi tena Kakonko, na hana hakika kama walikwisha kurudi Dar-es-Salaam walikotoka, au la! Anaendelea kuwasubiri, akitamani kuhojiwa!

No comments