Wapangaji kumfukuza pasta kwenye chumba cha muumini wake wa kike usiku




Pasta mmoja katika kijiji cha Matendeni mjini Embu alitimuliwa katika ploti moja na wapangaji nyakati za usiku kwa kuwapigia kelele alipokuwa akifanya kesha ya maombi na muumini wake wa kike.

Iliripotiwa kuwa wapangaji walishindwa kushitiri kelele za pasta huyo aliyefika kwa binti huyo kumuombea ili mumewe aliyepotea arejee nyumbani.

Binti huyo ambaye hakutajwa jina aliamua kutafuta huduma za pasta wake baada ya mumewe kukosa kurejea nyumbani kwa muda mrefu.

Kipusa huyo aliamini kuwa mumewe alitupiwa ndumba na kumfanya kumsahau, hali iliyopelekea mhubiri wake kukubali kuja kwake kwa kesha ya maombi.

Wapangaji walidai kuwa pasta huyo alipikiwa chakula kitamu kabla ya kuanza maombi yake kutokana na harufu iliyotokea katika nyumba ya binti huyo.

Mdokezi wa taarifa hii alisema kuwa pasta huyo alianza kumwombea binti huyo saa nne usiku kwa sauti ya juu.

Wapangaji walijaribu kuvumilia kelele hizo zilizowanyima usingizi, lakini walipoona kuwa maombi hao hayakai kuwa na mwisho, waliamshana na kwenda kumfukuza mhubiri huyo kutoka kwenye ploti hiyo.

Mpangaji mmoja alinukuliwa na gazeti la Taifa leo akifoka kuhusu kelele za mhubiri huyo walipokuwa wakielekea kwa nyumba ya binti husika.

“Pasta huyu hana adabu hata kidogo. Hatutamruhusu akeshe plotini hapa akipiga kelele eti anaombea muumini wake.” Mpangaji mmoja alisema wakibisha mlango wa binti huyo na kukatiza maombi yao ghafla.

Kipusa huyo alipofungua mlango, wapangaji hao wenye ghadhabu walimburura mhubiri huyo wakimrushia matusi na kumwondoa katika nyumba ya binti huyo. Walimzomea wakimwambia aliwaharibia amani ya kupata usingizi.

“Hatutakubali utuhabirie usingizi. Ulikuwa na muda wa kuomba tangu ulipoingia hapa. Sasa ondoka kwa sababu unapiga kelele sana na watu wanataka kulala.” Wapangaji walimwondoa mhubiri huyo aliyekuwa na Biblia mikononi mwake.

Kipusa aliyekuwa akiombea alijaribu kumtetea mhubiri wake lakini wapangaji hawakumsikiliza. Waliondoshwa pasta kwenye ploti hiyo, wakamtupwa nje na wakafunga lango kuu na kurejea katika nyumba zao.

Binti aliyekuwa akiombea aliachwa kinywa wazi na kuvunjwa moyo kwa sababu alitumai kuwa maombi hayo yaliyokatizwa yangemsaidia mumewe kurejea nyumbani.

Haijulikani ikiwa kipusa huyo aliyelenga kumpata mumewe aliandaa maombi mahali kwingine na mhubiri huyo au maombi yao yalisambatishwa na wapangaji wenzake.

No comments