SWEDEN YATOA BILIONI 195.5 KUSAIDIA ELIMU TANZANIA

Serikali ya Sweden imeipatia Tanzania Sh195.95 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ya Mpango wa Elimu kwa Matokeo (EPforR II).

Fedha hizo zilizotolewa kupitia Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Sweden (Sida), zitatumika katika mpango huo wa miaka mitano kuanzia Julai mwaka huu hadi Juni 2026.

Mpango huo umelenga kuongeza usawa wa upatikanaji elimu kwa wasichana na wavulana, watoto wanaotoka katika mazingira magumu na wenye ulemavu.

Akizungumza wakati wa kusaini mkataba huo, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Emmanuel Tutuba alisema awamu ya kwanza, mpango ulifanya vizuri na awamu hii, unakwenda kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili sekta ya elimu nchini.

Balozi wa Sweden nchini, Anders Sjoberg alisema licha ya mambo mengi kufanyika katika elimu, bado sekta hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

Alisema awali, wakati msisitizo ukiwekwa zaidi kwa wasichana katika utekelezaji wa awamu ya kwanza ya EPforR, ilishuhudiwa wavulana wengi wakiacha shule katika umri mdogo.

No comments