COSOTA YAKEMEA VIKALI USAMBAZAJI WA KAZI ZA FILAMU, MUZIKI

Taasisi ya Hakimiliki Tanzania COSOTA imekemea vikali usambazaji wa kazi za Muziki, Filamu na kazi zingine zote zinazolindwa na Sheria ya Hakimiliki usiozingatia utaratibu wa kisheria ikiwemo kudurufu na kusambaza kazi hizo pasipo makubaliano na mmiliki wa kazi hiyo.

COSOTA imesisitiza kuwa itachukua hatua kali za kisheria kwa watu wote watakaobainika kuzalisha na kusambaza kazi za Sanaa bila kuwa na vibali vya wamiliki sababu huo ni uharamia.

Hivi karibuni baada ya Mmliki wa Rekodi Lebo ya Kings Music na Msanii wa Muziki Alikiba kutoa taarifa ya kupatikana kwa albamu yake ya "Only One King' katika majukwaa mbalimbali ya mitandao ya kusambaza kazi za Muziki 'Digital platform kumeibuka watu wanaodurufu kazi hiyo na kuuza mitaani pasipo makubaliano yoyote na yeye COSOTA Imesema hili ni kosa kisheria.

"Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki namba 7 ya Mwaka 1999 imeeleza kuwa kusambaza kazi ya mbunifu yoyote bila ridhaa yake ni kosa kisheria na adhabu yake ni faini isiyopungua shilingi milioni ishirini au kifungo cha miaka mitatu mpaka mitano au vyote kwa pamoja"

COSOTA imetoa wito kwa wazalishaji na wasambazaji wote nchini kuacha kuzalisha na kusambaza kazi zote ambazo hazijazingatia sheria na ni lazima kuheshimu kazi za wabunifu na uwekezaji wanaofanya katika kuandaa na kuzalisha kazi hizo, imesema hali hii ya uharamia inachangia dhoofisha ukuaji wa sekta ya Sanaa nchini na kupoteza mapato ya wasanii.

"Tuheshimu ajira za wasanii na watunzi, tuache tabia ya kutaka kufaidika na jasho lao bila malipo ama makubaliano nao, COSOTA simamieni sheria, wakiukaji wa sheria wachukuliwe hatua, wadau ipeni COSOTA/Serikali ushirikiano kupambana na uharamia wa kazi za sanaa."---- Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Innocent Bashungwa

No comments