BILIONI 10.4 ZATENGWA KUJENGA VYUMBA VYA MADARASA ARUSHA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Ummy Mwalimu amesema Mkoa wa Arusha umepata takribani Bil 10.4 za Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 513.

Akitoa salamu za Ofisi ya Raia TAMISEMI mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan mapema leo amesema wanafunzi wote 42,000 wanaotegemewa kuanza kidato cha kwanza mwaka 2022 wataanza kwa awamu moja hakuna mtoto atakayechelewa kwa sababu ya uhaba wa vyumba vya madarasa.

Mhe. Ummy alitumia fursa hiyo kumshkuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzindua Hospitali ya Jiji la Arusha iliyogharimu Bil 2.5 na kukabidhi hundi za mikopo kwa vikundi zenye thamani ya shilingo Bil 1.3.

Aliwapongeza Halmashauri ya Jiji la Arusha kwa udhibiti mzuri wa Mapato ya ndani na kwa namna waliyoweza kuelekeza sehemu ya mapato hayo kutatua kero za wananchi na kutoa mikopo mikubwa kwa vikundi.

“Arusha mmefanya vizuri kwenye utoaji wa Mikopo kwa Vikundi hii ndio mikopo inayostahili kutolewa kwa Wananchi ,mikopo mikubwa yenye tija na sio vimikopo vidogo vidogo Rais Samia anataka kuona Vijana wanapewa Mil 100 au Wanawake wanapewa Mil 200 ili waweze kufanya vitu vikubwa vyenye tija vitakayoongeza uchumi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.”

Pia aliwataka madiwani wa Halmashauri za Mkoa wa Arusha kutokuzembea kutokana na upatikanaji wa fedha hizo bali wasimamie ukusanyaji wa mapato ili waweze kuendelea kununua madawati na mahitaji mengine muhimu ya shule.

Alimalizia kwa kuweka wazi Bajeti ya Mkoa wa Arusha ya Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kwa mwaka 2021/22 kuwa ni Bil 19.7 ukilinganisha na Bajeti ya mwaka 2020/21 iliyokuwa Sh Bil 9.8 tu.

No comments