SLAA, GWAJIMA, POLEPOLE WAHOJIWA NA KAMATI YA CCM

Wabunge watatu wa CCM Jerry Silaa (Ukonga), Askofu Josephat Gwajima (Kawe) na Humprey Polepole (mbunge wa kuteuliwa), leo Ijumaa Septemba 3, 2021 wamefika mbele ya kamati ya maadili ya wabunge ya CCM na kuhojiwa ikiwa ni kuitikia agizo la Bunge.

Wa kwanza kuwasili katika viwanja vya  makao makuu alikuwa Silaa aliyeingia hapo saa 3.57 asubuhi akiwa na gari nyeupe aina ya Toyota Harrier. Baada ya kushuka alionekana kuwa mwenye uso wa furaha, alikwenda moja kwa moja katika ukumbi wa ‘White House’.

Askofu  Gwajima na Silaa wameitwa na kamati kwa agizo la Bunge, wakidaiwa kusema uongo na kushusha hadhi ya Bunge,  ingawa haikufahamika Polepole ameitwa kwa agizo la nani.

Haikujulikana mara moja kuhusu ratiba waliyopangiwa,  lakini Silaa hakusimama nje wala kuongozana na mtu kuingia ndani ya ukumbi kama ilivyokuwa wakati akihojiwa bungeni.

Saa 4.47  Polepole alitoka ndani ya ukumbi na moja kwa moja akaingia kwenye gari lake akiwa na dereva wake na kisha wakaondoka.

Kabla ya kutoka, waandishi waliokuwa eneo hilo walimfuata mbunge huyo kutaka kuzungumza naye, lakini aliongea  kwa ufupi akisema:

"Kikao cha maadili ni kikao cha ndani, kwa hiyo taarifa zote zitatoka kwa utaratibu wa chama, nawashukuru sana," amesema Polepole na kuondoka eneo hilo.

Gwajima aliingia White House saa 5.28. Wakati huo Silaa hakuwa ameitwa ndani, alikuwa sehemu ya mapumziko ambako walisalimiana na kukaa pamoja wakisubiri wito.

Wakati wa mapumziko ya chai walionekana baadhi ya wabunge walioko kwenye kamati ya maadili akiwamo Deo Sanga, Maria Kisangi, Rashid Shangazi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais George Mkuchika.



No comments