ZANZIBAR WAANZA KUPOKEA CHANJO YA COVID-19

Wahudumu wa afya visiwani Zanzibar wameanza kupokea dozi ya kwanza ya chanjo ya covid-19. Serikali ya Zanzibar imethibitisha kuwa dozi za Sinocav kutoka nchini China zimeanza kutolewa kwa awamu ya kwanza huku awamu ya pili ikitarajiwa kufanyika baada ya wiki mbili kutoka sasa.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Ahmed Mazrui, amesema wameanza kutoa chanjo ya COVID-19 kwa Wahudumu wa Afya wa Hospitali za Serikali, Uwanja wa Ndege wa Abeid Karume na Bandari ya Malindi.

kwa upande wake, Katibu wa Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Omary Dadi Shajak amesema; ‘’Tumeanza kutoa chanjo wiki iliyopita kwa wahudumu wetu wa afya, tunawapa chanjo ya Sinovac kutoka China ambayo imepitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Tuna wahudumu wa afya elfu sita lakini kwa sasa tutaanza na nusu yao.

Kwa mujibu wa Dkt. Shajak chanjo hiyo awali ilipangwa kutolewa kwa mahujaji waliokua waende Makka, lakini kutokana na kuzuiwa kwa mahujaji kutoka nje ya Saudi Arabia, Wizara hiyo imeamua kutumia chanjo kwa wahudumu wa Afya.

Mpango huo wa chanjo hata hivyo unawalenga wahudumu wa afya wa Zanzibar pekee. Dkt. Shajak ameongeza pia chanjo ya pamoja na Tanzania bara itatolewa kwa utaratibu maalum kupitia mpango wa Covax.

No comments