WIZARA YA HABARI YAMPONGEZA RAIS SAMIA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Innocent Bashungwa Julai 06, 2021 amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumaliza siku 100 kazini kwa kishindo na mafanikio makubwa .

Mhe. Bashungwa amesema hayo wakati akifungua kikao cha kimkakati cha Menejimenti ya Wizara hiyo kilichoketi kujadili mikakati ya utekelezaji wa kazi za Wizara kwenye kipindi cha miezi sita ili kuleta mapinduzi makubwa kwenye sekta na wadau mbalimbali.

“Ndugu zangu dhamira ya kikao hiki ni kujipanga kimkakati ili kumsaidia Mhe. Rais kwenye dira aliyotuelekeza katika kipindi hiki ili matokeo yaliyokusudiwa yaweze kupatikana.” Ameongeza Mhe. Bashungwa.

Mhe. Bashungwa amesema amependa ubunifu wa kuwa na nguzo maalum zinazoongoza utekelezaji wa kimkakati uliofanywa na Mwenyekiti wa Menejimenti ya Wizara ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Hassan Abbasi, na Naibu wake Dkt. Ally Possi ambapo ametaka kila nguzo iwe na mkakati kabambe wa utekelezaji wake ili malengo yaweze kufikiwa.

Amesisitiza kuwa vikao hivyo vitakuwa ni sehemu ya kufanya tathmini na ufuatiliaji wa utekelezaji wa maelekezo ya Viongozi Wakuu wa nchi na kazi mbalimbali za Wizara.

Kwa upande wake, Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul amepongeza kazi zinazofanywa na Menejimenti ya Wizara na kutaka pia kuharakisha kutekeleza mikakati ya michezo kwa upande wa wananwake hapa nchini na vazi la taifa.

Awali, Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi akitoa maelezo ya utangulizi kwa Mhe. Waziri na Naibu wake Mhe. Pauline Gekul amesema nguzo tano  zimeainishwa ili kusaidia utekelezaji wa mikakati hiyo.

Amezitaja nguzo hizo kuwa  ni pamoja na  kuwafikia wadau mbalimbali ili kutatua changamoto, kufanya mageuzi ya kitaasisi na ya kiutendaji pamoja na kubadili mitazamo ya watendaji wa Wizara na taasisi zake.

No comments