WALIORASIMISHWA MAKAZI KUCHANGAMKIA FURSA SABASABA

Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt Angeline Mabula amewataka wakazi wa Dar es Salaam na Pwani waliorasimishiwa makazi yao kutumia fursa ya Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa kujipatia hatimiliki za ardhi zinazopatikana ndani ya siku moja katika maonesho hayo.
 
Akizungumza wakati wa kutembelea Banda la Wizara ya Ardhi katika maonesho hayo katika viwanja vya Mw. Nyerere vilivyopo barabara ya Kilwa Dar es Salaam Dkt Mabula alisema maonesho ya Sabasaba ni fursa nzuri kwa wananchi wa mikoa ya Dar es salaam na Pwani kujipatia hatimiliki za ardhi pamoja na huduma nyingine za sekta hiyo kwa uharaka zaidi.

Katika Maonesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa ya mwaka huu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inatoa hatimiliki za ardhi kwa wale wananchi waliorasimishiwa makazi yao na kuwa na nyaraka muhimu kupata hati ndani ya siku moja.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri Mabula, kasi ya serikali ya awamu ya sita ni kubwa na sasa hatimiliki ya ardhi inapatikana kwa siku moja tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo pamoja na mmiliki kuwa nyaraka zote lakini kupata hati ilikuwa vigumu.
 
"Kasi ya serikali ya awamu ya sita ni kubwa sana katika kuhakikisha migogoro ya ardhi inapatiwa ufumbuzi na kwa kuwa hivi sasa tuko katika mfumo wa kidigitali hatimiliki ya ardhi unaweza kuipata ndani ya muda mfupi kwenye banda la wizara hapa sabasaba tofauti kabisa na miaka ya nyuma" alisema Dkt Mabula.

No comments