Raisi Magufuli"Mungu kawaumbua wote"
RAIS John Magufuli amesema, Mungu amewaumbua watu waliodhihaki hatua ya serikali kufanya mazungumzo na Kampuni ya Bharti Airtel International mwaka mmoja uliopita.
Rais Magufuli ametoa kauli hiyo leo tarehe 10 Juni 2019, Ikulu Jijini Dar es Salaam wakati kampuni hiyo ikikabidhi hundi ya Sh. 3 Bilioni ikiwa ni gawio pamoja na Sh. 2.7 Bilioni kuunga mkono juhudi za serikali katika maendeleo
“Wapo waliodhihaki, waliocheka, waliojua hiki hakiwezekani lakini ninafikiri watu wote waliotutakia mabaya Mungu amewaumbua, kwasababu mazungumzo haya yamefikia mwisho,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amesema, mazungumzo hayo yamezaa matunda, ikiwemo kampuni ya Airtel ambayo itaigawia serikali Sh. 1 Biloni kila mwezi, katika kipindi cha miezi 60 mfululizo, fedha hizo zikikusanywa zitakuwa Sh. 60 Bilioni.
Amesema, fedha hizo zikipatikana zitasaidia kuboresha huduma za kijamii, ikiwemo uboreshaji wa huduma ya afya kwa kujenga vituo vya afya.
Wakati huo huo, Rais Magufuli amewapa pole viongozi walioapishwa leo Ikulu, akiwemo Dk. Edwin Mhede, Kamishna wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Innocent Bashungwa, Waziri wa Viwanda na Biashara, akisema kwamba majukumu yaliyo mbele yao ni makubwa.
“Nina wapongeza lakini nawapa pole, unajua Watanzania wanahitaji matokeo, ukitaka maneno mazuri kaelezwe na mke wako au mume wako.
“Sisi tunahitaji matokeo mazuri, mimi jukumu langu ni kuteua ili kusidi kiu ya Watanzania wanayohitaji ijitokeze, na ninapokutengua usifikiri nakuchukia nakupenda tu,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amewataka walioapishwa kutowachekea watu akisema kwamba, ni bora wachukiwe na watu kwa ajili ya utendaji kazi wao utakao mfurahisha yeye aliyewateua.
Chanzo :mwahalisionline
Hapa kazi tu
ReplyDelete