SERIKALI KUWEKA MAZINGIRA SAFI KUKUZA SEKTA YA VIWANDA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo amesema Serikali imepanga kuweka mazingira bora ili kuendeleza na kukuza Sekta ya Viwanda na Biashara ili iwe na mchango mkubwa katika pato la Taifa.

Waziri Mkumbo ameyasema hayo alipokuwa akiwasilisha mpango wa utekelezaji wa bajeti pamoja na maeneo ya ushirikiano yaliyopo katika Sekta ya Viwanda na Biashara katika Kikao cha pamoja kati ya Serikali na Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa nchini kilichofanyika Jana 12/07/2021 Benki Kuu, jijini Dar es Salaam.

Akiwasilisha maeneo ya ushirikiano katika kikao hicho kililcholenga kuwapitisha wajumbe hao katika Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Serikali ya mwaka 2021/22, Mipango ya utekelezaji pamoja na maeneo ya ushirikiano, Prof. Mkumbo amesema Tanzania itaendeleza makubaliano ya kibiashara baina ya Nchi na Nchi, Kikanda na Kimataifa kupitia majukwaa mbalimbali ya kibiashara ili kukuza biashara ndani na nje ya nchi.

Akitaja vipaumbele 10 vilivyoainishwa katika Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Bajeti ya Wizara kwa mwaka 2021/22 pamoja na programu 15 za utekelezaji, Prof. Mkumbo amesema, Wizara imeanzisha mpango maalum wa kuhamasisha bidhaa zinazozalishwa nchini kutumika nchini na kuongeza uzalishaji wa bidhaa hizo kwa ajili ya mauzo ya nje ya nchi.

Aidha, Prof Mkumbo amesema kuwa Serikali inachukua hatua mbalimbali katika kuboresha mazingira na kurahisisha ufanyaji biashara nchini ikiwemo kurekebisha sheria mbalimbali pamoja na kubadili mtazamo na utendaji kazi wa watumishi katika sekta hiyo ili kuwawezesha na kutoa huduma bora kwa wafanyabiashara.

Waziri Mkumbo pia amewasihi wajumbe wa kikao hicho kuendelea kisaidia sekta binafsi ambayo bado ni changa ili iweze kufanya biashara kwa ufanisi kwa kuzingatia sheria na weledi ili kukuza uchumi wa nchi.

Kikao hicho kilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Waziri wa Fedha na Mipango, Waziri wa Maliasili na Utalii, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu - Uwekezaji, Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa Nchini.

No comments