MUONGOZO WA KUSOMA BIBLIA LEO 22

LESONI LEO

ALHAMISI, JULAI 22,2021

 *WANAOAKISI NURU YA MUNGU* 

Pengine jambo la kawaida kwetu la kufanya baada ya kupambana na kushindwa kunakofadhaisha na kupitia uzoefu wa msamaha ni kujaribu kusahau kwamba tukio hilo liliweza kutokea. Kumbukumbu za kushindwa zinaweza kuwa za kuhuzunisha.

Daudi anataka kufanya nini na uzoefu wake wa kuhuzunisha? Soma Zaburi 51:13—19.

Wakati bakuli au chombo cha thamani kinapoanguka na kuvunjika vipande vipande, kwa kawaida tunashusha pumzi na kuvitupa vipande vilivyovunjika. Huko Japani kuna sanaa ya kitamaduni inayoitwa kintsugi, ambayo ni maalumu katika kuumba upya vyombo vya udongo. Madini ya thamani, kama vile dhahabu ya kimiminika au fedha, vinatumika kuunganisha pamoja vipande vilivyovunjika na kubadilisha chombo kilichovunjika kuwa kitu cha kupendeza na cha thamani.

Kila wakati Mungu anaposamehe makosa yetu na kutuumba upya tena, kitu kinabadilika. Msamaha wa Mungu wa thamani unaunganisha pamoja kuvunjika kwetu, na mipasuko inayoonekana huivutia neema Yake. Tunaweza kuwa vipaza sauti vya Mungu. “Na ulimi wangu utaiimba haki yako” (Zab. 51:14) Hatujaribu kujifanyia matengenezo binafsi au kupiga hatua binafsi (hata hatua kwa hatua). Roho zetu zilizovunjika, mioyo yetu yenye toba, ni sifa tosha kwa Mungu—na ni miali ya nuru ambayo dunia inaweza kuiona imetuzunguka. Uzoefu wetu wa kusamehewa huwavuta wengine wanaotafuta msamaha.

Kuna uhusiano gani kati ya Zaburi 51 na 1 Yohana 1:9?

Yohana wa kwanza —1 Yoh 1:9 ni ufupisho wa Zaburi 51. Daudi akiwa anajua kwamba “Moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau” (Zab. 51:17), Yohana anatuhakikishia kwamba, “Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote” (1 Yn. 1:9). Tunaweza kumwamini Mungu.

Tena, Daudi asingerekebisha uharibifu mkubwa sana alioufanya kutokana na matendo yake na mfano kwa familia yake. Alikabiliana na matokeo ya maamuzi na matendo yake. Na bado, Daudi alijua kwamba alikuwa amesamehewa. Alijua kwamba alihitaji kutumaini kwa imani kwamba siku moja Mwana-kondoo wa kweli wa Mungu angekuja na kusimama katika nafasi yake.

Unawezaje kujifunza sasa hivi kuzitumia ahadi hizi za 1 Yohana 1:9 katika maisha yako binafsi? Unapaswa kuhisije baada ya kufanya hivyo na kujua kwamba ahadi hiyo ni kwa ajili yako, pia?

No comments