JOB NDUGAI AWATAKA MA RC KUTOKULEWA MADARAKA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, amewataka wakuu wa Mikoa kote nchini, kuacha tabia yakulewa madaraka na kuonea watu bali wakafanye kazi zao kwakuzingatia misingi ya utawala bora.

Spika Ndugai ameyasema hayo leo Julai, 03, 2021, wakati akifunga mafunzo ya Uongozi yaliyo andaliwa na Taasisi ya Uongozi kwa Uratibu wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, ambapo Jumla ya Wakuu wa Mikoa 26 na Makatibu Tawala wa Mikoa yote 26 wamepatiwa mafunzo hayo kwa muda wa siku tatu jijini Dodoma.

“Kasimamieni Sheria, taratibu na kanuni za utumishi wa umma, msiende kumuonea mtu, kawatumikieni matajiri na masikini bila kujali uwezo wao wa kifedha” amesisitiza Spika Ndugai.

Ndugai, amewataka viongozi hao kutoruhusu urasimu, na badala yake wawe  watu wanaopatikana ili wananchi waweze kuwafikia kwa urahisi kufikisha kero zao, kwakuwa wao kama wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala, jukumu lao kubwa nikuangalia hali ya Usalama katika Mkoa, hivyo katika Mikoa ipo Migogoro mingi, na suluhu pekee ni kwa kuwasikiliza watu wanao waogoza.

Katika hatua nyingine Mhe. Ndugai, amewataka viongozi hao kwenda kusimamia rasilimali za umma kwa weledi, na maarifa walionayo pamoja na kudumisha mahusiano mema.

“Nendeni Mkadumishe mashirikiano baina yenu pamoja na taasisi zingine zote mnazo shirikiana nazo kwa namna moja au nyingine, epusheni migongano ya ninyi kwa ninyi katika maeneo yenu” Mhe. Ndugai.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. @ummymwalimu, akimkaribisha Spika Ndugai kufunga Mafunzo hayo, alimhakikishia Spika Ndugai kuendelea kushirikiana na mhimili huo wa Bunge katika kusukuma gurudumu la maendeleo.

“Mhe. Spika, Wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa hawa ndio wasimamizi wakubwa wa mambo yanayo pitishwa na Bunge, hivyo sehemu ya Mada ambayo wamefundishwa ni pamoja na mahusiano na taasisi zingine, tunaimani kabisa baada ya mafunzo haya ushirikiano huu unakwenda kudumishwa” alisema Waziri Ummy.

Naye Katibu wa Wakuu wa Mikoa, ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Martin Shigella, kwa niaba ya wakuu wa Mikoa na Makatibu Tawala wa Mikoa wameahidi kuyaishi yale yote waliyojifunza.

No comments