DKT. ABBASI AAGIZA COSOTA KUSIMAMIA HAKI ZA MB DOGG

Wizara ya Habari kupitia kwa Katibu Mkuu Dkt. Hassan Abbasi imeiagiza Taasisi ya Hakimiliki Nchini (COSOTA) kufuatilia na kuhakikisha msanii Mb Dogg anapata haki zake kutoka kampuni ambazo zimetumia kazi zake bila yeye kupata chochote.

Dkt. Abbasi ametoa maagizo hayo leo Dar es Salaam alipomwita msanii huyo aliyekuwa amelalamika kwenye mitandao ya kijamii akiomba msaada wa kupiganiwa haki zake.

“Hili limeisha COSOTA simamieni msanii huyu apate haki zake kutoka kampuni za ZIIKI na kampuni nyingine iitwayo ZEZE ambayo iko Kenya hivyo mtawasiliana mara moja na wenzetu wa Kenya kuhakikisha kazi za Mb Dogg zinapata stahiki yake,” alisema Dkt. Abbasi.

Msanii Mb Dogg ambaye alilalamika mitandaoni na kuwataja viongozi wa Wizara akiwaomba kumsaidia amesema amekuwa katika juhudi za kurejea kimuziki lakini alishangazwa na kubaini kuwa nyimbo zake nyingi zinatumika katika mitandao ya kuuza muziki bila aidha makubaliano au pale penye makubaliano bila kupewa stahiki zake.

Dkt. Abbasi pia ameitaka COSOTA kuendelea kuweka Kanuni zinazowalinda wasanii wa nchini huku akisisitiza uwazi katika makampuni yanayouza kazi za muziki.

Kwa upande wake msanii Mb Dogg ameishukuru Serikali kwa kuingilia kati swala hilo na anaamini kupitia Serikali kwa sasa anaweza kupata haki yake.@dktabbasi

No comments