BILIONI 9.6 KUSAMBAZA UMEME PEMBEZONI MWA JIJI LA MWANZA

Serikali kupitia Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) imetenga jumla ya takriban Shilingi bilioni 9.6 zitakazotumika katika mradi wa kusambaza umeme mijini (Periurban) katika mitaa ya pembezoni mwa jiji la Mwanza ikijumuisha Wilaya za Ilemela, Nyamagana na Misungwi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani Julai 9,2021 alipokuwa akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi huo wa awamu ya pili ya kusambaza umeme maeneo ya pembezoni mwa miji na majiji katika eneo la Shule ya msingi Igogwe iliyopo Kata ya Shibula wilayani Ilemela jijini Mwanza.

“Hatimaye kilio cha muda mrefu cha wana Mwanza kimesikika na Serikali ya Rais Samia Suluhu na tumewaletea umeme wa gharama nafuu ya Shilingi 27,000/- kama ilivyo kwa vijijini, niwasihi kuutumia umeme huu kujikwamua kiuchumi na kimaendeleo” alisema Dkt. Kalemani.

Dkt. Kalemani aliendelea kwa kuwataka Wakandarasi wanaosambaza umeme vijijini na TANESCO kuhakikisha wanatumia nguzo za zege hasa maeneo yenye changamoto ambazo ni imara na zinadumu kwa muda mrefu ukilinganisha na nguzo za miti ambazo hudumu kwa kipindi kifupi na huhitaji matengenezo ya mara kwa mara, matengenezo ambayo hupelekea kukatwa kwa umeme kupisha matengenezo hayo.

Dkt. Kalemani alimalizia kwa kuwataka Wakandarasi wote walioshinda zabuni za kusambaza umeme chini ya TANESCO na REA kuhakikisha wanatumia wazawa wa maeneo ambayo wanatekeleza miradi hiyo ili kuchochea ukuaji wa uchumi maeneo hayo na kuongeza ajira.

Naye Mbunge wa Ilemela, Dkt. Angelina Mabula alielezea furaha yake kubwa na wananchi kutokana na kiasi cha fedha kikubwa kilichotengwa kufanikisha miradi ya umeme wilaya ya Ilemela na maeneo mengine ya Jiji la Mwanza.

No comments