BIASHARA YA MADINI YA TANZANITE IFANYIKE MAREKANI-MAJALIWA

Waziri Mkuu Majaliwa Kassim Majaliwa  amemuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila kuhakikisha kuwa hadi kufikia tarehe 10 mwezi huu awe amefanya marekebisho ya kanuni za sheria ili wanunuzi wote wa madini ya Tanzanite wafanye biashara hiyo eneo la Mirerani.

Amesema kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kuwa madini hayo yanasimamiwa kikamilifu ikiwa ni pamoja na kuijulisha Dunia kuwa yanatoka Tanzania pekee na si kwingineko sambamba na kuwanufaisha wakazi wa eneo hilo na Tanzania kwa ujumla.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Julai 7, 2021) alipozindua Kituo cha Pamoja cha Magufuli kilichopo Mirerani, mkoani Manyara.

"Eneo hili lina umasikini mkubwa, inatakiwa mji huu uwe na thamani ya kitu chenyewe kinachotoka hapa, kila kitu Lazima kifanyike hapa hapa Mirerani, Tanzanite yote inunuliwe Mirerani"

Pia, amemuagiza Katibu Mkuu huyo kuhakikisha anawapatia vyumba wanunuzi katika jengo jipya alilolizindua ili wafanye biashara zao.

Amesema kuwa haiwezekani ujengwe ukuta wa kuzunguka eneo la mgodi wa Mirerani halafu madini hayo yatolewe na kwenda kuuzwa sehemu nyingine.

Kadhalika, Waziri Mkuu amewapa miezi mitatu wanunuzi wa Tanzanite kuhakikisha wanaanza kuongeza thamani madini hayo ikiwa ni pamoja na kujenga viwanda vya kuchakata madini hayo katika eneo la Mirerani.

"Sheria yetu inasema Tanzanite haiwezi kutoka nje ya nchi bila kuongezwa thamani, tukianza kuruhusu maeneo ya kuongeza thamani nje ya Mirerani ni rahisi kutoroshwa kabla ya kuongezwa thamani"

Amesema kuwa mpaka kufikia tarehe 15 Oktoba, 2021 wanunuzi wote wawe wameweka mitambo ya kuongeza thamani katika eneo la Mirerani na Serikali itatoa ardhi katika eneo Maalum la EPZA ili kuwawezesha kujenga viwanda vya uchakataji.

No comments